Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU SEKTA YA UKARIMU NA UTALII WAASWA KUSHIRIKIANA NA VETA KUBORESHA UTOAJI MAFUNZO


Wadau wa Sekta ya Ukarimu na Utalii wameaswa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ili kuboresha utoaji huduma katika sekta hiyo.

Ushauri huo umetolewa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Rebecca Nsemwa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, tarehe 29 Novemba,2024 wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Sekta ya Ukarimu na Utalii mkoani Dodoma.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Ofisi ya VETA Kanda ya Kati kwa kushirikiana na chuo cha VETA Dodoma, lilikuwa na lengo la kuwakutanisha wadau wa sekta ya ukarimu na utalii na chuo cha VETA Dodoma ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Nsemwa amesema Dodoma, ikiwa ni kitovu cha shughuli za Serikali sasa inakua kwa kasi kubwa kiuchumi na kijamii, ambapo ukuaji huo unaibua fursa nyingi katika sekta mbalimbali, mojawapo ikiwa ni Sekta ya Ukarimu na Utalii.

“Sote ni mashahidi kuwa hoteli na nyumba za kulala wageni zinaendelea kujengwa sambamba na uhitaji wa huduma nyingine kama chakula, vinywaji na kumbi za mikutano nao ukiongezeka. Kwa hivyo, uendeshaji wa shughuli hizo unawategemea ninyi wadau wa sekta ya Ukarimu na Utalii,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, amewaomba washiriki wa kongamano hilo kujadili na kutoa maoni kwa uwazi kuhusu huduma na mafunzo yanayotolewa na VETA na namna kushirikiana katika kuboresha utoaji mafunzo na huduma kwa ujumla.

Amesema, uboreshaji wa huduma katika Sekta ya Ukarimu na Utalii utasaidia kukuza utalii na kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutangaza utalii kama alivyofanya kupitia Sinema yake ya Royal Tour, iliyotangaza na kuhamasisha utalii.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa VETA na wadau kutoka sehemu za kazi katika mafunzo utasaidia kukuza umahiri wa wanafunzi na hatimaye kupata wahitimu wenye stadi bora ambao watatoa huduma zenye kiwango cha kimataifa katika sekta ya ukarimu na utalii.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhan Mataka ametoa rai kwa wadau wa ukarimu na utalii kushirikiana na VETA Dodoma katika kutafuta fursa za kibiashara pamoja na kutatua changamoto zinazolalamikiwa katika sekta hiyo.

Amesema, angefurahi kuona wadau wa sekta ya utalii wanabadilishana uzoefu na VETA katika kuwanoa vijana wanaohudumia wageni wanaoingia na kutoka katika jiji la Dodoma.

“Tungependa kuona meneja wa hoteli fulani anakuja kuwafundisha wanafunzi wa ukarimu na utalii, vivyo hivyo Mwalimu wa ukarimu kutoka VETA anaenda kuwafundisha watoa huduma hotelini”, Mataka amesema.

Kongamano hilo liliwahusisha wadau zaidi ya 100 kutoka Sekta ya Ukarimu na Utalii wakiwemo watoa huduma za Hoteli, kumbi za sherehe na mikutano, mama lishe, watoa huduma za vinywaji na waokaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com