NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Kata ya Kilungule, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, wameiomba serikali kudhibiti utitiri wa vikundi na taasisi zinazotoa mikopo chechefu na kupelekea mkopaji kufilisika pindi akichelewesha rejesho.
Akizungumza leo Desemba 13, 2024 Jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo na Vituo vya Taarifa na Maarifa Kata ya Kilungule, Mkazi wa Nzasa A, Bi.Ngibwa Mwambona amesema kwa kiwango kikubwa mikopo hiyo, inatolewa kiholela bila masharti magumu na kina mama ndio wakopaji wakubwa ambao huishia kulipa riba kubwa.
Amesema mikopo hiyo haina lengo la kuwasaidia wananchi hususan wanawake kujikwamu kiuchumi badala yake inalenga kunyonya uchumi wao.
“Tunaiomba serikali kuingilia kati suala la mikopo umiza katika jamii zetu , kila eneo inatolewa na hakuna mlolongo mrefu wa kupata fedha zao, masharti yake ni nafuu, wanawake wake wanakimbilia huko na baaadae kuanza kulipa kwa riba kubwa,” Amesema
Nae Shaban Ramadhan ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kwa Mzungu, amesema kuwa kwa kiwango kikubwa mikopo hiyo, inawaathiri kwa sababu baadhi ya wanawake hawawashiriki pindi wanapohitaji kukopa.
Aidha amesema kuwa uwepo wa vikundi vingi vya kukopesha katika mitaa yao, kumechangia wanawake kuingia tamaa ya kupata fedha kwa njia rahisi.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Wilaya hiyo, Furaha Chiwile, amewasisitiza wanawake kuachana na mikopo umiza badala yake, wajiunge kwenye vikundi vinavyotambulika ili kunufaika na fedha za asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri bila riba.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkuu wa Kitengo cha Tehema, Yahya Madenge mesema kwa mujibu wa sheria wao, hawana mamlaka ya kufuta au kuondoa taasisi hizo, badala yake, watafanya mazungumzo nao ili kuangalia namna ya kupunguza riba zao ili zisiwaumize wananchi.
Social Plugin