Wananchi na wafanyakazi wa Serikali wa Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wamejitokeza kwa wingi katika Kituo cha Afya cha Mjimwema kilichopo ndani ya manispaa hiyo, kwa kufanya usafi kama sehemu ya kuadhimisha Sherehe za Uhuru.
Diwani wa Kata ya Mjimwema Silvester Mhagama akishirikiana na viongozi wa serikali wameongoza zoezi hilo la usafi.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhagama amesema hatua hiyo imelenga kuwashirikisha wananchi na wagonjwa wanaopatiwa huduma kwenye kituo hicho katika sherehe za kitaifa za Uhuru.
Amesema usafi umelenga kuboresha mazingira ya kituo cha afya na kuonyesha mshikamano wa jamii, hasa katika siku ya kuadhimisha uhuru wa taifa.
Mhagama amewashauri wananchi waliojitokeza katika kituo hicho kutumia fursa ya kuwa katika mazingira ya afya kwa kupima afya zao, akisisitiza umuhimu wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali zao za kiafya.
Aidha, Mhagama ameipongeza serikali na viongozi kwa kufanya kazi kwa weledi na kujitolea kwa maslahi ya taifa, akisema kwamba tunapaswa kuenzi na kutunza rasilimali za taifa letu, kwani "hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania yetu."
Amehimiza pia wananchi kuendeleza utamaduni wa kujitokeza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ili kuimarisha mshikamano na utamaduni wa kuwa pamoja katika shughuli za maendeleo.
Social Plugin