Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewasili katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE ) kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE tangu kuanzishwa kwa uhusiano huo mwaka 1974.
Baada ya kuwasili nchini humo Mhe. Waziri Kombo , amefanya kikao cha maandalizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini UAE ulioko jijini Abu Dhabi.
Mhe. Waziri Kombo ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Majadiliano ya Kwanza ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE yatakayofanyika jijini Abu Dhabi tarehe 5 Desemba, 2024.
Katika Majadiliano hayo Tanzania na UAE zitajadiliana kuhusu utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kati ya pande mbili hizo.
Mhe. Waziri Kombo pia anatarajiwa kutoa mhadhara katika Chuo cha Diplomasia cha nchini UAE cha Anwar Gargash Diplomatic Academy utakaofanyika tarehe 4 Desemba, 2024 ambapo atawasilisha mada kuhusu miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Tanzania na UAE na matarajio ya baadae.
Mhe. Waziri pia ashiriki katika hafla maalum ya kusherehekea Siku ya UAE itakayofanyika tarehe 5 Desemba, 2024 ambayo imeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE.
Vilevile, Mhe. Waziri atashiriki katika majadiliano ya kibiashara yatakayohusisha wafanyabiashara wa Tanzania na UAE yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhusiano kati ya Tanzania na UAE, Mhe. Waziri pia anatarajiwa kuwa na mikutano ya uwili na Viongozi wa Serikali ya UAE kwa minajili ya kuendelea kuimarisha Uhusiano na Ushirikiano na Serikali ya UAE.
Maadhimisho haya yanatarajiwa pia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Uvuvi hususan katika eneo la Bahari Kuu na Uchumi wa Buluu, chanjo za mifugo na binadamu na uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea.
Tanzania na UAE zinashirikiana kupitia sekta za nishati, Kilimo, mifugo, anga , elimu, kazi, viwanda, biashara, uwekezaji na miundombinu.