Waziri Silaa ametoa maagizo hayo leo tarehe 16 Desemba,
2024 wakati akizindua Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), jijini
Dar es Salaam.
Amesema kuwa maagizo hayo yanakuja kufuatia maelekezo
mahsusi yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, tarehe 10 Desemba, 2024, Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar wakati
wa hafla ya uapisho wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Naibu Makatibu Wakuu na
Mabalozi kuhusu usimamizi wa shirika hilo kujiendesha kibiashara.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Bodi na menejimenti ya
Shirika la TTCL, Waziri Silaa amesema, "Serikali ya Rais Dkt. Samia
imewekeza fedha nyingi katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo mkongo wa
taifa wa mawasiliano, minara ya mawasiliano, pamoja na kituo cha kuhifadhia
data cha taifa (National Data Center).
"Nia ya Rais ni kuona uwekezaji huu mkubwa
unaleta tija nchini." Amesema Waziri Silaa na kuongeza;
"Shirika hili likiendeshwa vyema lina uwezo wa
kusaidia sekta nyingine, kwa sababu wizara yetu ni wezeshi katika mawasiliano,
hivyo wizara nyingine na Taasisi zinaitegemea katika kukuza sekta zao za
TEHAMA."
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL Bw. David
Nchimbi amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua kuongoza bodi hiyo na kuahidi
kusimamia shirika ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Bw. Nchimbi amemshukuru Waziri Silaa kwa utayari alioonesha na kuahidi kuwa bodi itatoa ushirikiano kwa wizara wakati wote itakapokuwa inatekeleza majukumu yake.