Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Shirika la Abilis Foundation lenye makao yake makuu nchini Ufaransa limefadhili Mradi wa Kuimarisha Uongozi kwa Watu Wenye Ulemavu utakaotekelezwa na Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope inayoendesha shughuli zake Dodoma.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Foundation For Disabilities Hope, Michael Salali wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mradi huo unaogharimu shilingi milioni 40 za Tanzania unalenga kuwafikia watu 300 wenye ulemavu katika wilaya ya Kondoa.
Amesema mradi huo utawalenga wanawake na wasichana kwa kuwajengea uwezo katika uongozi na ujasiriamali ili kuwa na jamii yenye mtazamo chanya wa mabadiliko ya kuwapa nguvu wanawake na watu wenye ulemavu kwenye nafasi za kutoa maamuzi.
Ametaja gharama za mradi huo kuwa ni shilingi milioni 40 ambapo ameeleza kuwa kwa jumla, mradi huo utaleta mabadiliko ya kipekee katika wilaya ya Kondoa kwa kuimarisha haki za binadamu na kutoa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika jamii na uongozi.
"Taasisi yetu inatamani kuona jamii inaimarika na kuwa na mtazamo chanya wenye matumaini kwa wenye ulemavu,mradi huu utaongeza uelewa na kuhamasisha jamii ya Kondoa kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu na jinsi wanavyoweza kuwa viongozi bora, hivyo kutengeneza mazingira bora kwa ushirikiano wa watu wote, "amesema.
Ameeleza kuwa mradi huo utakuza maendeleo ya kiuchumi kwa watu wenye ulemavu na kufafanua kuwa watakapokuwa na uongozi imara, wataweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao, hasa katika maeneo ya kiuchumi, na kuboresha hali ya maisha ya watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla.
"Watu wenye ulemavu watapata nafasi ya kuwa viongozi wa mfano kwa jamii zao, na kuwaonyesha wengine kwamba ulemavu haukupi kikwazo cha kufikia malengo ya juu katika maisha, " amesema
Salali ametaja faida zitakazotokana na Mradi huo kuwa ni pamoja na kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika uongozi ambapo mradi utasaidia watu wenye ulemavu kushiriki katika nafasi za uongozi, hasa katika ngazi za kijamii na kisiasa, na hivyo kuboresha uwakilishi wao katika jamii.
Faida nyingine ni kuboresha usawa wa kijamii kwa kuwezesha watu wenye ulemavu kushika nafasi za uongozi ambapo mradi utachangia kupunguza ubaguzi na kuhamasisha jamii kuhusu haki na usawa kwa watu wote, bila kujali hali zao za ulemavu.
"Tunatajaria mengi zaidi kupitia huu mradi ikiwemo kuongeza uwezo na ujuzi,mradi utatoa mafunzo na rasilimali muhimu kwa watu wenye ulemavu, kuwapa ujuzi wa uongozi, mawasiliano, na usimamizi wa miradi, hivyo kuwajengea uwezo wa kujiongoza na kusaidia wengine, "amesema.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Foundation for Disabilities Hope Furaha William,amesema kwa kuanza mradi huo utaanza kutekelezwa Wilayani Kondoa na kueleza sababu za kuichagua wilaya hiyo kuwa imekuwa ikisahaulika katika miradi mingi ya maendeleo.
"Mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii kwa kuimarisha ushiriki wa watu wenye ulemavu na wanawake katika uongozi, " ameeleza
Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utahamasisha na kuchochea zaidi ushirikiano wa makundi mbalimbali kati ya taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wadau wengine ili kuboresha mazingira kwa watu wenye ulemavu, hivyo kuleta manufaa kwa jamii nzima.
“Mradi huu umekuja kwa wakati muafaka, hasa baada ya uchaguzi mdogo na kuelekea uchaguzi mkuu,tunataka kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kujitokeza kuchagua na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila kujihisi wanyonge,” amesema na kuongeza;
Tunataka kuonyesha kuwa wanawake wenye Ulemavu wanaweza kutoa maamuzi makubwa,tunaye role model wetu Rais Samia Suluhu Hassan,wote tunamtazama kama kiongozi na mfano mzuri wa uongozi bora,” amesema Furaha
Social Plugin