Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZIARA YA SEKTA YA MAJI KOREA KUSINI YAFANIKISHA MRADI WA MAJITAKA DAR ES SALAAM

 


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema ziara iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea Kusini imetengeneza mahusiano mazuri na kuchangia kupatikana kwa fedha kwa ajili ya mradi mikubwa wa majisafi na usafi wa mazingira.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Mfumo wa Kutibu Majitaka Katika Jiji la Dar Es Salaam kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam ( DAWASA) na Mkandarasi kampuni ya Kolon Global Corporation kutoka inchini Korea Kusini kwa ufadhili wa Korea Exim Bank ikiwa ni siku chache baada ya Ziara ya Waziri Aweso na timu nzima ya sekta ya Maji Nchini Korea Kusini.

"Baada ya kupata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alifanya ziara inchini Korea Kusini baadae na mimi nikapata nafasi safari hizo zimepelekea tumepata zaidi ya Dola za kimarekani zaidi ya milioni 240 kwa ajili ya uwekezaji kwenye miradi ya usafi wa Mazingira" amesema Waziri Aweso

Ameongeza kuwa hiyo inathibitisha mahusiano mazuri na urafiki wa thamani uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemshukuru Balozi wa Korea Kusini nchini Mhe. Eunju Ahn kwa kuwa sehemu kubwa ya kusaidia kupatikana kwa ufadhili wa miradi hiyo.

Zoezi hilo la utiaji saini limeshuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwenye kikao kazi cha mafunzo kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa ambapo alisisitiza ushirikishwaji wa viongozi kuanzia ngazi za mitaa kwani ni muhimu kwa wao kuwa na taarifa sahihi ili kurahisisha uwasilishaji kwa wananchi.

Naye, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire akitoa maelezo wa mradi amesema mradi utahusisha ujenzi wa mtambo mkubwa wa kisasa wa kuchakata majitaka eneo la Buguruni, Ujenzi wa vituo viwili vikubwa vya kusukuma majitaka eneo la Gymkana na Jangwani, 

Ameongeza kuwa utahusisha pia kazi ya ulazaji wa bomba kubwa kwa umbali wa zaidi ya kilomita 52 na ukarabati wa mfumo uliopo wa majitaka, Mradi unategemea kunufaisha wakazi 733,865 katika Wilaya za Ilala na Kinondoni.

Mradi huo utagharimu zaidi ya dola milioni 90 sawa na bilioni 170 fedha za kitanzania mpaka utakapokamilika ambapo Waziri Aweso amesema itakuwa suluhisho kubwa kwa changamoto za maji katika hilo kukamilika kwake kutaongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa jiji la Dar Es Salaam kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 65"

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com