Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Modest Mkude, amekabidhi gari la wagonjwa wa dharura aina ya Land Cruiser pamoja na pikipiki mbili (Yamaha) kwa ajili ya kusaidia utoaji wa chanjo kwa mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Makabidhiano hayo yamefanyika Januari 3, 2025, katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha.
Mhe. Mkude amesisitiza kuwa watumiaji wa vyombo hivi wavitumie kwa malengo ya kazi elekezi ili kufikia malengo ya serikali, hasa kuhakikisha chanjo inapatikana kwa wote.
Ameongeza kuwa hadi mwaka 2024, huduma ya chanjo ilitekelezwa kwa 83%, na malengo ya mwaka 2025 ni kufikia 100% na zaidi.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi kwa kuwapatia wananchi huduma bora. Huduma hii itasaidia kwa usafiri wa wagonjwa na kusambaza chanjo kwa wananchi," amesema Mhe. Mkude.
Aidha, Mhe. Mkude amepongeza kitengo cha chanjo kwa jitihada zao, akisema hajawahi kupata malalamiko kuhusu usambazaji wa chanjo na huduma za afya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu, ameipongeza serikali kwa utekelezaji wa ilani ya chama, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu na ufanisi kwa watumishi wa afya ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa haraka.
Kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Godfrey Kisusi, ameishukuru Serikali kwa kutoa gari na pikipiki, akisema kuwa usafiri wa dharura utapunguza usumbufu wa muda mrefu wa kusubiri magari ya wagonjwa.
Kisusi pia ameeleza kuwa katika mwaka 2024, huduma ya chanjo imefanikiwa kwa 95% kupitia mfumo wa "chanjo ya mkoba", huku chanjo kwa watoto ikiwa imetolewa kwa 83%. Serikali pia ilitoa shilingi milioni 70 kwa ajili ya kusaidia kuwafikia watoto waliokosa chanjo.
Baadhi ya wananchi wa Kishapu, akiwemo Eliufoo Vema, wamepongeza serikali kwa kutatua changamoto za vifo vya mama na mtoto, akisema kuwa gari hilo litaleta mabadiliko makubwa, hasa katika maeneo yenye miundombinu mibaya.
Hata hivyo, Fikiria Mathius, mkazi mwingine wa Kishapu, ameomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara, kuongeza magari ya dharura, na kuongeza idadi ya watumishi wa afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Gari la dharura litakabidhiwa kwa Kituo cha Afya cha Ng'wanghalanga kilichopo Kata ya Masanga, na kuongezea magari ya dharura sita katika Wilaya ya Kishapu.
Taarifa ya chanjo ya 2024 inaonyesha kuwa huduma za chanjo zinaendelea vizuri, huku idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma ya chanjo ikiwa ni 59 kati ya 64 vilivyopo, na huduma za mkoba zikiwa zinafanyika katika jumla ya vituo 1092 kila mwaka.
Social Plugin