Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MACHA KUZINDUA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA SHINYANGA JANUARI 25


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali akizungumza na waandishi wa habari - Picha na Malunde

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga yatazinduliwa rasmi Januari 25 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha. Utoaji wa elimu ya sheria katika maadhimisho hayo utatumika utaratibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao.

Hayo yamebainishwa leo Januari 20, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema siku ya Sheria huashiria mwanzo wa kuanza kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka mpya husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza kila tarehe 15 Desemba na kumalizika Januari 31 ya mwaka unaofuata, ili kuanza rasmi utendaji kazi wa utoaji haki.

Amesema uzinduzi rasmi wa Wiki ya Sheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga utafanyika Januari 25 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katika viwanja vya Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga, na itahitimishwa rasmi Februari 1 katika Viwanja vya Mahakama Kuu.

“Kwa kuzingatia kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanafanyika siku za kazi, ambapo wananchi wengi watakuwa katika shughuli za utafutaji wa kipato, utoaji wa elimu kwa mwaka huu umelenga kuwafuata wananchi karibu zaidi na maeneo yao wanayofanyia kazi, tofauti na ilivyokuwa hapo awali,” amesema Jaji Mfawidhi Mahimbali.

“Elimu hii ya kisheria tutaitoa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kwa kutumia magari maalumu yatakayokuwa yanahama kutoka eneo moja kwenda jingine. Pia, tutaongeza wigo wa utoaji elimu kwenye maeneo ya shule za msingi, sekondari na vyuo,” ameongeza Mahimbali.

Amesema ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi zaidi, watatumia pia vyombo vya habari kupitia luninga, redio na mitandao ya kijamii.

Amesema katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria, pamoja na mambo mengine, elimu hiyo itachagizwa pia na Tamasha kubwa la bonanza la michezo kwa Watumishi wa Mahakama katika ukanda huo.

Pia, amesema katika Wiki ya Sheria, kauli mbiu itakayokuwa ikijadiliwa ni “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai Katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Amesema kauli mbiu hiyo inawasaidia kutumia mkakati na utekelezaji wa maboresho ya Mahakama, hasa wanapoiendea dira mpya ya matumaini ya mafanikio 2050, ya uchumi wa kiwango cha kati ngazi ya juu. Na kwamba wao Mahakama wamejipanga kufanikisha mpango huo na watakuwa watekelezaji wakuu wa Dira hiyo ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali akizungumza na waandishi wa habari - Picha na Malunde
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali akizungumza na waandishi wa habari
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali akizungumza na waandishi wa habari

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com