Hivi karibuni, tumeshuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikimthibitisha kwa kauli moja na kwa asilimia 100 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, kuwa mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Kama ilivyo katika sheria zetu, kila baada ya miaka mitano, uchaguzi hufanyika kwa ngazi ya Urais, Ubunge, na Udiwani. Katiba ya 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaainisha kuwa taifa letu ni la kidemokrasia, na hivyo uchaguzi huu ni matakwa ya kikatiba.
Historia ya Uapisho wa Viongozi, Hasa Rais wa Nchi
Historia inaonyesha kuwa Marais wote tangu uhuru mwaka 1961 hadi 2022 wameapishwa katika Jiji la Dar es Salaam, Uwanja wa Uhuru, na Rais Samia aliapishwa Ikulu ya Magogoni mwaka 2022.
Ifahamike kuwa mwaka 1973 lilipitishwa azimio la kutambua kuwa Dodoma ndio makao makuu ya nchi yetu, ingawa serikali iliendelea kufanya kazi Dar es Salaam hadi 2017 ilipohamia Dodoma rasmi.
Hivi sasa, serikali, idara zote, na Ikulu pia zimejengwa na kumalizika Chamwino, Dodoma. Aidha, mji wa serikali wa Mtumba, maarufu kama "Magufuli City," umeendelea kukamilika na kuanza kutumika.
Nchi yetu ni ya mfumo wa vyama vingi, hivyo uchaguzi huu utakuwa wa ushindani. Hata hivyo, mgombea wa tiketi ya CCM, Rais Samia, bila shaka ataibuka mshindi.
Kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Ndg. Steven Waisira
Siku ya tarehe 18, akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma, Ndg. Steven Wasira alisema, "CCM haina sababu ya kushindwa uchaguzi, kwa kuwa sababu za kushinda zipo, uwezo wa kushinda upo, na kwa kuanzia, CCM ina idadi ya wanachama milioni 12.5 ambao wamesajiliwa kidigitali."
Sababu nyingine ni huduma bora za kijamii, miundombinu, amani na ulinzi ulioimarika, pamoja na mtandao mkubwa wa mabalozi hadi ngazi za mashina. Hivyo, tunaposema Rais Samia ataapishwa Dodoma, tunathibitisha kuwa ana nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huu.
JE, RAIS SAMIA KUAPISHWA DODOMA?
Ni vigumu kubainisha wazi kama Rais Samia ataapishwa Dodoma au Dar es Salaam. Tunajiuliza: Je, ni lazima uapisho ufanyike Dodoma au Dar es Salaam? Kwani haiwezekani uapisho wa kiongozi mkuu wa nchi ufanyike katika mkoa mwingine, mfano Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar au Mtwara? Haya ni maswali tu ambayo majibu yake yanaweza kupatikana kwa usaidizi wa mtaalamu wa sheria.
Kama mwandishi na mtu mwenye maono, naamini Rais Samia ataapishiwa Dodoma, na hivyo historia mpya itaanza kuandikwa kuanzia Oktoba 2025.
Kwanini Rais Aapishwe Dodoma?
Kusadifu Makao Makuu ya Serikali: Makao makuu ya serikali na taasisi zake zote zimehamia Dodoma kwa ukamilifu.
Kuvutia Balozi na Misheni za Kimataifa: Uapisho utahamasisha balozi na misheni za kimataifa kujenga ofisi Dodoma kwa haraka, ikizingatiwa kuwa sasa Dodoma ndio makao makuu ya serikali (embassies badala ya consulates).
Kuongeza Mvuto wa Dodoma: Uapisho utavutia mtazamo chanya kuhusu makao makuu ya nchi.
Kuongeza Miundombinu: Ujenzi wa miundombinu ya msingi kama vile mahoteli, kumbi za mikutano za kisasa, na huduma nyingine muhimu kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa.
Kuheshimisha Makao Makuu ya Serikali: Uapisho utaheshimisha makao makuu ya serikali na utulivu kwa watumishi wa umma, kuwa Dodoma ni makao makuu rasmi ya nchi.
Kuhamasisha Uwekezaji wa Kimkakati: Uapisho utahamasisha uwekezaji, mfano viwanda na makampuni makubwa kuhamia Dodoma. Mfano mzuri ni kiwanda cha Intracom Fertilizer kilichopo Nala, Dodoma.
Kwa uhalisia wake, kuna kila dalili za Rais Samia kuapishwa Dodoma, kwa kuwa mazingira ya Dodoma ni rafiki kwa wageni waalikwa, na viwanja vya kutosha kwa sherehe za kitaifa. Wakaazi wa Dodoma tuna shauku kubwa kuona siku hiyo, ambapo Rais wa nchi atapishwa katika ardhi ya Dodoma, ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitambua kama makao makuu ya serikali.
Rais Samia atakuwa Rais wa kwanza kuapishwa Dodoma, na pia kiongozi wa kwanza kukamilisha ndoto ya Baba wa Taifa ya kufanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Social Plugin