Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUKIA MUGEJWA MFANYAKAZI BORA WA TRA MKOA WA RUVUMA TRA AWARDS 2024/2025


 
Pichani washindi wa TRA Awards wakiwa pamoja na Rais Dkt. Samia na baadhi ya viongozi waliohudhuria tuzo hizo

Na Regina Ndumbaro Dar es Salaam. 

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza hafla ya utoaji wa Tuzo za TRA Awards 2024/2025  katika viwanja vya Mlimani City Dar es Salaam tukio ambalo lilifanyika kwa mafanikio makubwa.

 Hafla hii ya kihistoria iliyofanyika Januari 23,2024 iliandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutambua na kusherehekea mchango wa watendaji bora na walipakodi wenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.


Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wa kitaifa walihudhuria, akiwemo Waziri wa Fedha, Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, pamoja na wakuu wa mikoa na wadau wa sekta binafsi. 


Mgeni rasmi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ubunifu, na uwazi katika ukusanyaji wa mapato kama nyenzo muhimu ya maendeleo endelevu ya taifa huku akihimiza kuwa kauli mbiu ya sera yetu ya mapato Tanzania ni "Kodi yetu ni kwa maendeleo yetu sote".


Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo  hizo ni Rukia Mugejwa, ambaye alitangazwa kuwa Mfanyakazi Bora wa TRA kwa mwaka 2024/2025 akitokea katika Mkoa wa Ruvuma. 


Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rukia amesema, "Ninajivunia sana kutambuliwa kwa mchango wangu. Tuzo hii ni motisha kubwa siyo kwangu tu bali pia kwa wenzangu. Inatufundisha kwamba bidii, uaminifu, na kujituma vina thamani kubwa katika kazi zetu za kila siku."

Rukia ameongeza kuwa, ushirikiano mzuri kati ya wafanyakazi na uongozi wa TRA umechangia mafanikio haya. Ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya mamlaka hiyo. 

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa hafla ya chakula cha jioni, ambapo wadau walipata nafasi ya kujadili mbinu za kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, huku wakikumbushwa jukumu la kila mmoja katika kufanikisha maendeleo ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com