Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

STEPHEN WASIRA APENYA NAFASI YA MAKAMU MWENYEKITI CCM BARA

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, ameibuka mshindi kwa kishindo katika uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, baada ya kupata kura 1,910 zinazolingana na asilimia 99.42% ya kura zilizohesabiwa. 

Uchaguzi huu umefanyika katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa unaoendelea jijini Dodoma leo, Januari 18, 2025.

Msimamizi wa uchaguzi, ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa jumla ya kura 1,921 zilipigwa katika mkutano huo, huku kura halali zikiwa 1,917. Kura 7 zilikuwa za "Hapana", wakati kura 4 ziliharibika. Kura za "Ndiyo" zilikuwa 1,910, zikionyesha wazi msaada mkubwa kwa Wasira kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo. Hii ni asilimia 99.42% ya kura halali.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Wasira amewashukuru wajumbe kwa heshima kubwa waliyompa kushika nafasi hiyo huku akieleza kuwa kazi kubwa waliyonayo ni kushika dola na kudumisha muungano na kwamba atakuwa  mdau mkubwa wa maridhiano kwa sababu CCM ni chama cha amani.

"Asanteni sana kwa kunipa heshima hii, tuendelee na kazi iendelee",amesema Wasira.

Wasira, ambaye ni mzalendo na mbobevu wa siasa, amejiweka katika historia ya CCM na taifa kwa kujitolea kwake katika nyadhifa mbalimbali za uongozi,  aliyezaliwa Julai 1, 1945, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, amekuwa na mchango mkubwa katika siasa, uchumi na maendeleo ya jamii kwa zaidi ya miongo mitano.

Kwa zaidi ya nusu karne, Wasira amepata heshima kubwa kutokana na juhudi zake za kuimarisha taifa na chama. Ni miongoni mwa wana-CCM waliowahi kutangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wasira ni mmoja wa viongozi wakongwe wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM. Tangu mwaka 2007, amekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), na tangu mwaka 2011, ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Hii inamuweka katika nafasi ya kuendelea kuwa na sauti kubwa katika mchakato wa kisiasa wa chama hicho tawala.

Katika nafasi hii ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Wasira atakuwa na jukumu muhimu la kusimamia na kuratibu shughuli za chama katika upande wa Bara, na kusaidia kuimarisha uongozi wa CCM katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu 2025.

Kwa sasa, Stephen Wasira anakuwa sehemu ya uongozi wa juu wa CCM, ambapo atakuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha mikakati ya chama na kujenga uhusiano mzuri kati ya CCM na wananchi wa Tanzania Bara. 

Uchaguzi huu unamuweka Wasira katika nafasi muhimu zaidi ya kisiasa, akiwa na jukumu kubwa la kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya chama katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com