Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauter J. Kanoni
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauter J. Kanoni
Na Regina Ndumbaro Masasi .
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Lauter J. Kanoni, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shuleni mara moja baada ya kufunguliwa kwa shule.
Amezungumza hayo jana tarehe 22 Januari 2025 ofisini kwake, Kanoni amesisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto na wazazi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu.
Kwa upande wa Masasi Mji, mahudhurio ya wanafunzi wa darasa la kwanza yamevuka matarajio, ambapo wanafunzi 3,100 wameripoti, sawa na asilimia 109 ya makadirio ya wanafunzi 2,932. Aidha, wanafunzi wa darasa la awali walioripoti ni 2,614, sawa na asilimia 81 ya makadirio.
Kanoni amewapongeza wazazi wa Masasi Mji kwa mwamko huo lakini akaendelea kusisitiza umuhimu wa kufanikisha mahudhurio ya asilimia 100.
Hata hivyo, hali ya mahudhurio kwa shule za sekondari bado inahitaji msukumo wa ziada. Wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti Masasi Mji ni 1,420, sawa na asilimia 76 ya waliochaguliwa kujiunga.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni ili kufanikisha jitihada za serikali za kuboresha elimu ya sekondari.
Kwa upande wa Masasi DC, hali ya mahudhurio bado ni changamoto. Wanafunzi wa darasa la awali walioripoti ni 3,382, sawa na asilimia 49 ya makadirio ya wanafunzi 7,306. Aidha, wanafunzi wa darasa la kwanza walioripoti ni 3,608 kati ya makadirio ya wanafunzi 5,971, sawa na asilimia 60. Hali hiyo, kwa mujibu wa Kanoni, inahitaji ushirikiano mkubwa wa wazazi na viongozi wa shule kuhakikisha mahudhurio yanaongezeka.
Kwa shule za sekondari katika Masasi DC, wanafunzi 4,423 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025, lakini walioripoti ni 3,070, sawa na asilimia 69.4.
Kanoni amesisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni kabla ya tarehe 1 Machi 2025, na akatoa tahadhari kuwa wazazi watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mbali na suala la elimu, Kanoni amekemea tabia ya baadhi ya wakazi wa Masasi Mjini kulima mazao, hususan mahindi, ndani ya mipaka ya mji.
Amesema kitendo hicho ni kinyume na sheria za mipango miji na kinaharibu mandhari ya mji. Ameonya kuwa viongozi wanaoshindwa kusimamia agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mkuu huyo wa Wilaya alimalizia kwa kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha mazingira ya mji yanakuwa safi, salama, na watoto wote wanapata fursa ya elimu. Amesema jukumu la kufanikisha elimu bora ni la kila mmoja na linahitaji ushirikiano wa jamii nzima.
Social Plugin