Pichani Mhandisi Tarura Wilayani Tunduru Msola Julius akiwaangalia mafundi wanaojenga Daraja katika Barabara ya Mchoteka-Likweso-Wenje
Pichani kazi ya ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji kwenye Barabara ya Mchoteka-Likweso-Wenje wilayani Tunduru ikiendelea
Na Regina Ndumbaro Tunduru.
Wakazi zaidi ya 6,600 wa vijiji vya Mchoteka, Likweso, na Wenje wilayani Tunduru wamepata ahueni baada ya Serikali kutumia shilingi milioni 480 kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilometa 24 inayounganisha vijiji hivyo. Barabara hiyo imeondoa changamoto ya kukosa mawasiliano ya barabara ambayo iliathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa Mhandisi wa TARURA wilayani Tunduru, Msola Julius, barabara hiyo haikuwepo awali, hali iliyosababisha wakazi kushindwa kusafirisha mazao yao kama korosho, karanga, na mpunga. Amesema kuwa mradi huo umefungua fursa mpya kwa usafiri, usafirishaji wa mazao, na shughuli nyingine za kiuchumi kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Mhandisi Julius ameeleza kuwa kazi za ujenzi wa barabara hiyo zilianza rasmi tarehe 29 Mei 2024 na zinatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 24 Januari 2025. Kazi kubwa zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji yenye urefu wa kilometa 1.6, makalavati 12, na daraja moja. Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha mradi huo muhimu.
Amebainisha kuwa mbali na umuhimu wa kiuchumi, barabara hiyo ni muhimu pia kwa usalama, kwani vijiji hivyo vinapakana na nchi jirani ya Msumbiji. Barabara hiyo itasaidia katika kurahisisha mawasiliano ya haraka na kuimarisha ulinzi wa maeneo ya mipakani.
Mkandarasi wa mradi huo, Abdulrahman Soud kutoka Kampuni ya ARICOM ENTERTRADE, amesema kuwa mradi huo ulifanyika katika sehemu mbili kuu. Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kufungua barabara kwa kumwaga kifusi na kuweka makalavati, kazi ambazo zimekamilika kikamilifu. Sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa daraja, ambalo linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki mbili zijazo.
Soud amesema kuwa kufunguliwa kwa barabara hiyo kumewapa wakazi wa vijiji hivyo vitatu fursa kubwa ya mawasiliano na usafiri wa uhakika. Barabara hiyo itasaidia sana katika kusafirisha mazao ya wakulima kwa urahisi na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Omari Malenga, mkazi wa kijiji cha Mchoteka, amesema kuwa kabla ya ujenzi wa barabara hiyo, changamoto kubwa ilikuwa maji ya mvua yaliyokuwa yakisababisha mafuriko na kuharibu makazi yao. Pia, wakulima walikuwa na changamoto ya kusafirisha mazao kutoka shambani hadi sokoni, hali iliyopunguza tija yao kiuchumi.
Wananchi wa vijiji vya Mchoteka, Likweso, na Wenje wameipongeza Serikali kwa mradi huo na kusema kuwa barabara hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwao. Wamesema kuwa sasa wanaweza kusafirisha mazao yao, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, na kufanikisha maendeleo yao binafsi na ya kijamii.
Social Plugin