NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha kushindilia gesi asilia (CNG) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam .
Akizungumza katika ziara hiyo leo Januari 9, 2025 Jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko ameridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambapo ameeleza kwamba kukamilika kwa kituo hicho mapema mwaka huu kutawawezesha Watanzania kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Dkt. Biteko amesema kuwa kuanzia Februari 3 Mwaka huu, kituo hicho kitaanza kutoa huduma ya kujaza gesi asilia kwenye magari.
Aidha amesema kuwa serikali imeelekeza kujengwa kwa vituo vingine vya gesi asilia, ambapo vituo saba vya ziada vinajengwa na sekta binafsi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa Wizara ya Nishati imepanga kuanzisha vituo vinavyotembea vya kujaza gesi asilia katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kuwa wamekubaliana na Shirika la Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuleta mabasi yanayotumia gesi asilia hatua inalenga kuhamasisha Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuelekea kwenye nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho kimetoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo,Profesa William Anangisye amefafanua kuwa mradi huo utatoa fursa kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi kutumia kituo hicho kama sehemu ya mafunzo ya vitendo.
Social Plugin