Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UWAPIBATA WAKABIDHI FEDHA RAIS SAMIA ACHUKUE FOMU 'MITANO TENA'




Na Hadija Bagasha - Tanga

Chama cha umoja wa wamiliki na  waendesha pikipiki na bajaji Mkoa wa Tanga (UWAPIBATA) kimemkabidhi shilingi milioni moja mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Hamisi Mkoba ili kumsaidia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya urais mwaka huu. 

Akizungumzia uamuzi huo Mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amewapongeza bodaboda hao kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni moja kwajili ya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea urais Mwaka 2025. 

Fedha hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa bodaboda Wilaya ya Tanga Mohamed Chande kwa niaba ya bodaboda wengine na kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa CCM kwenye hafla ya Mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu wakati alipokutana na madereva wa bodaboda na bajaji jijini Tanga katika uwanja wa Lamore.

Mwenyekiti huyo amesema wanachama wake wanakabiliwa na changamoto ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiwasababishia vifo na ulemavu kutokana na ukosefu wa leseni na  elimu ya usalama barabarani. 

Kufuatia hali hiyo umoja huo umemuomba Mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu kusaidia kutunisha mfuko wao ili waweze kukabiliana na changamoto hiyo pamoja na kuwaongezea nguvu katika mfuko wao wa kukopeshana leseni za udereva. 

Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu ametoa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kuwasaidia waendesha pikipiki kukabiliana na changamoto hiyo. 

Katika kuendelea kuboresha mazingira rafiki kwa waendesha pikipiki Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema atashirikiana na wadau mbalimbali ili kila mtaa uwe na kituo cha bodaboda cha kiuchumi kwajili ya waendesha bodaboda .

"Nitahakikisha naacha alama kwa bodaboda kuna mdau nitashirikiana naye kujenga vituo vya bodaboda katika mitaa yote 181 ya Jiji la Tanga, hatutaita vijiwe vya bodaboda bali vitakuwa ni Bodaboda Resource Center humo tutaweka WiFi lakini bodaboda watasoma masomo ya jioni," amesema Ummy.

Ummy aliwapongeza bodaboda hao kwa kuguswa na kazi nzuri zilizofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumchangia fomu ya Urais mwaka huu Dkt Samia Suluhu Hasaan.

"Ndugu zangu wa bodaboda hongereni kwa kuguswa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumchangia fomu ya kugombea Urais, hongereni sana hili ni jambo kubwa mmelifanya na hakuna Mtanzania asiyeona kazi kubwa iliyofanywa na Rais wetu, amefanya kazi kubwa sana katika Jiji letu ikiwemo kutuboreshea bandari yetu na nyie ni mashahidi abiria wameongezeka kutokana na bandari," amesema.

Katika hafla ya kukutana na bodaboda na bajaji iliyofanyika katika uwanja wa Lamore jijini Tanga imeambatana na zoezi la kuwawekea mafuta pikipiki na bajaji zaidi 500 jijini Tanga. 
 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com