*Ni kuhusu kuwapeleka watoto shule, watakaokaidi kuchukuliwa hatua za kisheria
Na Lydia Lugakila - Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera Erasto Sima amewataka Wazazi kuwapeleka watoto wao walio na sifa za kujiunga na kidato cha kwanza, wanaoingia awali na Darasa la kwanza kupelekwa shule mara moja ili kuungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Samia Suluhu hassan katika sekta ya elimu.
Erasto Sima ametoa kauli hiyo Januari 13, 2025 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni msisitizo kwa Wazazi kuwapeleka watoto shule baada ya shule za msingi na Sekondari kufunguliwa Januari 13,2025.
Amesema kuwa Rais Samia ametengeneza miundo mbinu mizuri Katika shule mbali mbali Nchini ikiwemo za Mkoa wa Kagera huku akiendelea kutoa maagizo ya watoto kupelekwa shule agizo alilolitoa wakati akifungua shule nyingi huko visiwani Zanzibar wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar.
"Rais Samia ameendelea kutuagiza viongozi kuwa ni lazima wanafunzi wote wanapopangiwa shule waende kweli"alisema Dc Erasto.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa wazazi kuungana na Rais Samia katika suala la elimu kwani kazi hiyo sio ndogo licha ya kuwa wazazi hutofautiana katika vipato lakini hiyo haimkatazi mtoto kwenda shule.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa kwa Wilaya ya Bukoba yenye kata 29 tayari kidato cha kwanza ambao walikuwa wamefanya mtihani wavulana walikuwa ni 4,483 wasichana 4,749 na waliofaulu ni wavulana ni 3,050 na wasichana 3,348.
"Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba waliopangiwa kwenda kidato cha kwanza katika shule mbali mbali jumla ni 6,339 ambapo wavulana ni 3,028 wasichana ni 3,311"alisema kiongozi huyo.
Aidha alisema upo utaratibu wa kuchukua fomu kwa wanafunzi wanaoanza kusoma, zoezi ambalo lilianza wiki kadhaa zilizopita lakini hadi Januari 10,2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kati ya Wanafunzi 6,339 ni wavulana 2,340 waliochukua fomu na wasichana 2,440 jumla wakiwa 4,780 sawa na asilimia 75.
"Kwa Manispaa ya Bukoba wanafunzi waliokuwa wamechaguliwa na kupangiwa shule za Sekondari jumla ni 3,268 wavulana ni 1,524 na wasichana ni 1,744 huku waliochukua fomu wakiwa ni1,028 Wavulana na Wasichana 1,047 jumla 2,075 sawa na asilimia 63.4 jambo lililoonesha wengi kutochukua fomu.
Aliwahimiza wazazi waliochukua watoto katika shule binafsi kuwa huru ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ili ijulikane watoto walipo na kama wanaendelea vizuri.
Alichukua muda fursa hiyo pia kuwaomba wazazi kuwapeleka watoto wao kuanza awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza kabla ya hatua kali kuchukuliwa kwao huku akiahidi ifikapo Januari 17,2025 atapata taarifa ya waliofika shuleni na Januari 20 yeye na timu yake watafuatilia na kuchukua hatua ikiwa bado watakuwepo wazazi waliokaidi watakiona cha moto.
Hata hivyo Dc Sima aliongeza kuwa hata kama uchumi kwa wazazi sio mzuri Ila ataongea na wakurugenzi ili wawasiliane na Wakuu wa shule ili kuona namna ya watoto wao kuendelea kupokelewa ili kutokwama ki masomo wakati wazazi wao wanajiandaa huku akiahidi kuwa kwa mwaka 2025 hakuna mchezo juu ya watoto kutokwenda shule
Social Plugin