Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI MASANGA WAIPONGEZA SERIKALI KUPATA GARI LA WAGONJWA

Mbunge wa jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Boniphace Butondo akiwasha gari
Makabidhiano ya funguo na nyaraka za magari ya dharula yaliyotolewa na serikali Mbunge wa jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Boniphace Butondo akikabidhi kwa Kaimu mganga mkuu wa Wilaya hiyo Godfrey Kisusi Januari 7,2025 katika viwanja vya kituo cha afya Ngw'ahalanga kilichoko Kata ya Masanga

Mbunge wa jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Boniphace Butondo akizungumza na wananchi wa Kata ya Masanga baada ya kukabidhi funguo na nyaraka zingine gari la wagonjwa wa dharula kwa Kaimu mganga mkuu wa Wilaya hiyo Godfrey Kisusi walipokuwa katika kituo cha afya cha Ng'wanghalanga na nyingine kwenda kutumika hospitali ya Wilaya ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Januari 7,2025.


Na Sumai Salum - Kishapu

Baadhi ya Wananchi wa Vijiji vinavyounda Kata ya Masanga Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wameipongeza serikali ya awamu ya sita na Mbunge wa jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo kuwaboreshea huduma ya afya kwa kuwapa gari la wagonjwa wa dharula(ambulance).

Pongezi hizo zimetolewa Januari 7,2025 baada ya Mbunge kukabidhi funguo na nyaraka zingine za gari kwa Kaimu mganga mkuu wa Wilaya Godfrey Kisusi ambapo gari moja litasalia kituo cha afya cha Ng'wahalanga na lingine hospitali ya Wilaya ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete.


Mkazi wa Kijiji cha Kinampanda Nyanzobe Saida(18) amesema gari hilo litawasaidia wazazi pindi watakapopata matatizo ya uzazi wakati wa kujifungua na kuhitajika kutoka zahanati,kituo cha afya hadi hospitali ya Wilaya watafika kwa wakati na kwa usalama zaidi.


Naye mkazi wa kijiji cha Bulekela Sophia John ameipongeza serikali kwa kuipa hadhi na kuipendelea Kata hiyo kwani ni mwaka mmoja tangia kupandishwa kutoka zahanati kuwa kituo cha afya na hata sasa wamepata gari la wagonjwa wa dharula ambalo litasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto sambamba na wagonjwa wengine.


Hata hivyo, Mkazi wa kijiji cha Ngw'ahalanga Khamis Moses amesema ujio wa gari hilo la wagonjwa litawasaidia kupunguza gharama za kukodi usafiri wa magari kwa watu binafsi kwani wamekuwa wakitozwa fedha nyingi na wakati mwingine wakishindwa kuzilipa na hatimaye kuingia kwenye migogoro ya madeni.


Akizungumza wakati akikabidhi magari hayo Mbunge Boniphace Butondo amesema serikali ya awamu ya sita imejizatiti kuboresha sekta ya afya ili kupunguza na kuondoa vifo vya mama wajawazito,watoto na wagonjwa wengine.

"Mwaka Jana tulikuja na Ummy Mwalimu akiwa bado Waziri wa afya tulitembelea hospitali ya Wilaya nikamweleza changamoto za hospitali ya Wilaya na kituo cha afya Ngw'ahalanga na maeneo mengine nikamuomba baada ya gari moja watupe mawili alilifikisha kwa Rais Samia Suluhu na mimi nikaongeza msukumo Mungu amekuwa mwema tukakabidhiwa na Rais wetu mpendwa magari mawili" amesema Butondo.


Mhe. Butondo ameongeza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa gari hilo ili lifanye kazi iliyokusudiwa na endapo watumishi watalitumia vinginevyo wanapaswa kutoa taarifa kwa viongozi.


"Serikali imetoa gari imara linalopitika maeneo yote litatusaidia hata wakati wa magonjwa ya mlipuko na pia nina imani na Daktari Mfawidhi wa kituo hiki Dkt. Charles Mayala kuwa atalisimamia vizuri na kuhakikisha analitunza gari hili kusudi liendelee kudumu na kuwasaidia wananchi wa Kata hii na Kata zingine zinazohudumiwa na kituo hiki ikiwemo Lagana,Mwakipoya pamoja na Kata ya Somagedi", ameongeza.


Aidha,Mhe.Butondo amewapongeza wananchi kwa kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi CCM na ofisi ya Mbunge na kuwaahidi kipindi cha bunge kilichosalia ataomba fedha za upanuzi wa kituo hicho cha afya ili kuongeza nyumba za watumishi ambapo kwa sasa zipo nyumba mbili na watumishi nane,Jengo la kuhifadhia maiti,wodi pamoja na njia zinazounganisha jengo moja na jingine.


"Niwapongeze pia na ndugu zangu watumishi kwa moyo wenu wa kukubari kuja kufanya kazi huku vijijini kwenye mazingira magumu thawabu yenu iko mbinguni kwa kuwahudumia wananchi wetu, na pia wananchi muwatunze hawa watumishi muishi nao kama ndugu pamoja na sisi" ,ameongeza.

Aidha, ofisi ya Mbunge imeahidi kutoa mifuko 100 ya saruji ambayo itasaidia ujenzi wa jengo la nyumba ya watumishi huku akiwashauri kutembelea kituo cha afya Mwamalasa ili kuona ramani.


Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dr.Charles Mayara amepongeza juhudi za serikali,Mbunge na Diwani wa Kata hiyo katika sekta hizo kwani inasaidia kuboresha afya zao ili uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii uongezeke.
Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Godfrey Kisusi akizungumza baada ya kupokea ufunguo na nyaraka za gari kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Mhe.Boniphace Butondo Januari 7,2025 wakati wa kupokea gari la wagonjwa wa dharula katika kata Masanga




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com