Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WASHAURI BAJETI YENYE MTAZAMO WA KIJINSIA KUSAIDIA WATOTO NJITI





Mjumbe wa kamati ya Ufundi ya Mtandao wa Afya ya Uzazi, Dkt. Dinner Mbaga, akizungumza

Mkurugenzi Mtendaji wa WFT-T, Bi. Rose Marandu, akizungumza wakati wa mjadala

Na Deogratius Temba, Dar es salaam

Mtandao wa Haki ya afya ya uzazi umeshauri Serikali kutenga bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia katika sekta ya afya ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu na utunzaji wa watoto njiti wanapozaliwa.
 
Hayo yamesemwa na wanachama wa Mtandao wa haki ya Afya ya uzazi (SRHR) wakati wa mjadala wa pamoja kuhusu marekebisho ya sheria ya ajira, ambapo mswada wake unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni.
 
Akizungumza mjumbe wa Kamati ya kushughulikia ushawishi na utetezi kwenye mabadiliko ya sheria hiyo, ili kuwapa nafasi wanawake kupata likizo ya uzazi ya kutosha pindi wanapojifungua watoto Njiti, Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Moleli Foundation, Doris Moleli, alisema kwamba suala la uzazi wa mtoto njiiti ni lazima lijadiliwe na jamii kubadilisha mitazamo hasi, lakini kutenga bajeti katika ngazi za kijiji na kata ili zahanati na vituo vya afya viweze kuweka miundombinu na vifaa vya kusaidia kuhudumia watoto njiti katika ngazi hiyo.

“ ….Zanahati zetu na Vituo vya afya huko vijijini zikipewa rasilimali fedha na vifaa vya kuhudumia watoto njiti, itasaidia sana kuondoa tatizo. Wanawake wanaojifungua watoto njiti wanasafiri umbali kutoka vijijini , kutumia muda mrefu kufuata huduma hospitali kubwa na kusababisha umasikini miongoni mwa jamii kutokana na mzigo wa gharama”, alisema Doris.

Doris aliongeza kwamba, endapo serikali itatenga fedha za kutosha kwenye bajeti ya wizara ya afya, hususani katika kuwekeza kwenye kuhudumia mama wanaojifungua watoto njiti, sambamba na ununuzi za vifaa vya kuhudumia watoto hao, itapunguza mzigo wa kazi na kuondoa usumbufu na mzigo wa gharama za matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake (WFT-T), Rose Marandu alisema kwamba suala la kutenga rasilimali fedha kwenye bajeti za serikali ngazi zote ni la msingi na litaweza kuondoa kwa kiasi kikubwa umaskini, udhalilishaji na ukatili wa Kijinsia kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti.
 
“Mtoto wa haki ya afya ya uzazi una kazi kubwa kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa jamii, Jamii hasa wanaume ambao ni wadau wakubwa kwenye suala la uzazi washirikishwe kikamilifu na kuelewa wajibu wao ili mwanamke anapojifungua mtoto njiti, asinyanyasike, kudhalilishwa na kufanyiwa ukatili, lakini wanaume wanapaswa kutenga bajeti kwenye ngazi ya familia na kutoa muda wao kumsaidia mwenza kwenye kulea mtoto njiti”, alisema Marandu.

Mapendekezo ya Mtandao wa SHRSR kwenye muswada wa sheria ni kwamba kifungu cha 33 kilichopendekezwa kwamba likizo ya uzazi kwa mama aliyejifungua mtoto njiti, iongezwe na kuanzia wiki ya 36 ya ujauzito ambapo mtoto angepaswa kuzaliwa kawaida, ndipo ianze likizo ya kawaida, iongezwe hadi wiki ya 40 kwasababu wapo wanawake wanojifungua kawaida ambao hufikia wiki ya 40.

“Kifungu kina tija kwa wafanyakazi waliojifungua kabla ya muda ili kuruhusu mzazi kuhudumia mtoto kwa ukaribu ili atengemae ispokua siku zilizotajwa hapo ziongezeke kutoka wiki 36 mpaka wiki 40 kwa sababu za Kiafya hasa makuzi ya mtoto” ,alisema Dkt. Dinna Mbaga, ambaye ni Mjumbe katika kamati ya kiufundi ya Mtandao wa haki ya Afya ya Uzazi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com