Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI MBAMBABAY


Baadhi ya wakazi wa Mbambabay wakipita barabarani
Barabara ya lami Mbambabay

Na Regina Ndumbaro Ruvuma

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara katika mji mdogo wa Mbambabay kwa kiwango cha lami. 

Wakazi hao wamesema kuwa ujenzi wa barabara hizo umeboresha huduma za usafiri na usafirishaji, kuondoa changamoto za vumbi na matope, na kuongeza thamani ya maeneo yao.

Petro Zambala  ni  mkazi wa Mbambabay amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita, akibainisha kuwa ujenzi wa barabara hizo umeongeza kasi ya maendeleo na kuchochea uchumi wa wananchi mmoja mmoja na wilaya kwa ujumla. 

Ameongeza kuwa, kabla ya ujenzi huo, wananchi walipata changamoto kubwa kufika kwenye huduma za kijamii kwa wakati.

Nikaya Mbalale, mkazi mwingine wa mji huo, amesema kuwa fedha zilizotolewa na Serikali zimebadilisha kwa kiasi kikubwa miundombinu ya mji huo. Amesema barabara nyingi za mitaa zilikuwa za vumbi lakini sasa zimejengwa kwa kiwango cha lami, jambo ambalo limevutia wawekezaji wengi na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

Mbalale ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara ya Mbambabay-Mbinga yenye urefu wa kilometa 66 kwa kiwango cha lami kumeleta unafuu mkubwa kwa wananchi. Nauli ya kutoka Mbambabay hadi Mbinga imeshuka kutoka Shilingi 15,000 hadi kati ya Shilingi 9,000 na 10,000. Hii ni hatua kubwa katika kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

Jackob Madondola amebainisha kuwa, miaka ya nyuma, wananchi walikabiliwa na mateso makubwa kutokana na ubovu wa miundombinu, hususan katika kipindi cha masika. Amesema ujenzi wa mifereji ya kutiririsha maji sambamba na barabara za lami umesaidia kuondoa tatizo la mafuriko na kuwapa wananchi fursa ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa amani.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa, Derick Theonest, amesema kuwa wamebakisha kilometa moja tu ili kukamilisha mtandao wa barabara za lami katika mji wa Mbambabay. Ameshukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha ambazo zimewezesha kuboresha miundombinu, akisisitiza kuwa barabara hizo ni muhimu katika kuchochea maendeleo.

Wananchi wamehimizwa kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kwani imegharimu fedha nyingi. 

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kwa manufaa ya wananchi na kukuza uchumi wa maeneo ya vijijini na mijini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com