Katika hatua inayovutia na kuibua hisia mchanganyiko, Tundu Lissu amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akimshinda mtangulizi wake, Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea nafasi yake katika uchaguzi wa kihistoria uliofanyika Januari 21,2025 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Uchaguzi huu unafunga ukurasa wa miaka 21 ya uongozi wa Mbowe, ambaye ameiongoza CHADEMA kwa kipindi kirefu na aliyejizolea umaarufu mkubwa kama nguzo kuu ya upinzani nchini Tanzania.
Lissu, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa baada ya kurejea kutoka uhamishoni na kuwa kiongozi shupavu katika upinzani, ameongoza kampeni ya kushinda nafasi hiyo.
Hata hivyo, Mbowe amekubali matokeo kwa heshima, akimpongeza Lissu na kusema anajiandaa kuunga mkono uongozi wake mpya.
Licha ya matokeo ya jumla kutotangazwa baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu matokeo yatatangazwa baadaye, lakini ukumbini shangwe limetawala.
Msingi wa shangwe hilo ni kura za nafasi ya uenyekiti zimemalizika kuhesabiwa na mawakala wa Lissu kwa namna moja au nyingine wamepenyeza matokeo ya awali.
Katika ukurasa wake wa Mtandao kijamii wa X, Mbowe ameandika ujumbe wa kukubali kushindwa akiweka na picha aliyopiga na Lissu na kuandika:
"Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya Uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama chetu CHADEMA uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama", ameandika Freeman Mbowe
Kuchaguliwa kwa Lissu kunakuja wakati muhimu kwa CHADEMA, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko makubwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Lissu anaonekana kama kiongozi mwenye mvuto na msimamo mkali dhidi ya utawala wa sasa, na chama kinatarajia kuimarika zaidi chini ya uongozi wake.
Kwa upande wa Mbowe, kumaliza kwa uongozi wake ni ishara ya demokrasia ndani ya CHADEMA, ambapo mabadiliko ya kisiasa yanapatikana kwa njia ya amani na heshima.
Social Plugin