Na Lydia Lugakila - Kagera
Mbunge wa Bukoba vijijini Mkoani Kagera Dkt. Jasson Rweikiza amekabidhi gari la kubebea Wagonjwa lenye thamani ya Shilingi Milioni 400 katika kituo cha Afya Katoro kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ikiwa ni utimizaji wa ahadi ya Rais Samia baada ya kilio cha gari hilo kwa muda mrefu.
Akizungumza Januari 25, 2025 kabla ya kukabidhi gari hilo kwa uongozi wa kituo cha Afya Katoro na Wananchi wa kata ya Katoro Mbunge Rweikiza amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu hassan kwa kuwaona wana katoro kwani changamoto ya gari la kubebea wagonjwa ilikuwa ni kilio kwao kwani kila vilipoitishwa vikao mbali mbali agenda ilikuwa gari la wagonjwa hii ni kutokana na lililokuwepo kuwa bovu na kutumia zaidi ya shilingi Milioni 12 kila likifanyiwa ukarabati.
Mbunge Rweikiza aliwasisitiza Watumishi wa kituo hicho kulitunza vizuri gari hilo kwa ajili ya lengo kusudiwa la kuwahudumia wagonjwa na si vinginevyo kwani nia ya Rais Samia ni kuona Wananchi wanafurahia huduma bora.
"Vituo vilikuwa ni vingi ambavyo havina gari la wagonjwa lakini Rais Samia kakiona kituo cha katoro nawaomba sana gari hili litumike kwa kazi moja ili lidumu kwa muda mrefu likae hapa lisubiri wagonjwa na si baada ya kazi jioni linatumiwa na watu binafsi, linapakia mizigo angalieni msije rudi tulipotoka"alisema Rweikiza.
Aidha amempongeza Diwani wa kata ya Katoro kwa kupaza sauti yake kila kukicha kuhusiana na ubovu wa gari la wagonjwa hadi Rais Samia kuona na kusikia kisha kutenda.
Vile vile mbunge huyo alisema anatamani Katoro iwe bora zaidi ambapo tayari ameisha kamilisha baadhi ya matakwa ya Wananchi ikiwemo mradi wa maji uliokuwa kero kwa muda mrefu ambao unakwenda kukamilika hivi karibuni ili Wananchi wapate maji safi na salama pia uboreshaji wa barabara katika baadhi ya maeneo, ambapo katika sekta ya Elimu wamefanikiwa kujenga shule zikiwemo za Sekondari, uwekaji taa za Barabarani, kuwezesha kituo cha Afya Katoro kuwa na jenereta baada ya umeme kukatika katika kila mara, uboreshaji wa madaraja likiwemo la Karebe na Kyanyabasa ambayo yanakwenda kukamilika na kurahisisha shughuli za Wananchi kwa haraka.
Akisoma taarifa ya kituo cha Afya Katoro mganga mfawidhi Dkt Luckson Kagumisa alisema kituo hicho kongwe kilianzishwa mwaka 1943 na kinahudumia kata takribani 8 kwa Bukoba vijijini pamoja na kata jirani ya Wilaya ya Misenyi huku akiishukuru Serikali kwa kuwapatia gari hilo kwani litarahisisha utoaji wa huduma za rufaa kwa wagonjwa kutoka Katoro kwenda Hospitali ya Wilaya hiyo na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pia kusafirisha wagonjwa kutoka Zahanati hadi kituoni hapo ambapo pia amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya.
Kwa upande wake Mkurungezi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Fatna Laay ameshukuru ujio wa gari hilo huku akikili kuwa gari lililokuwepo mara nyingi lilikuwa linaharibikia njiani likiwa na wagonjwa na kusababisha wakati mwingine wagonjwa kufia njiani huku akimshukuru Diwani wa kata hiyo aliyefikisha kilio hicho kwa mbunge wa jimbo la Bukoba vijijini naye kumfikishia Rais Samia.
Naye Diwani wa kata ya Katoro Haruna Hamed amemshukuru mbunge huyo na Serikali ya awamu ya sita kutokana na utekelezaji katika sekta mbali mbali kwa maeneo mengi sio tu ya Afya huku akimshukuru Mkurungezi mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa ushirikiano mzuri katika utendaji wake wa kazi pamoja na mbunge huyo.
Hata hivyo nao Wananchi wa kata ya Katoro na maeneo mengine akiwemo Zaifath Ismail, Hassan Husein, Yahya Aziz jirani waliokuwepo katika hafla hiyo fupi ya kukabidhiwa gari walisikika kwa shangwe nyingi na vigelegele wakimpongeza Rais Samia mbunge huyo kwa kutatua kero hiyo.
Social Plugin