Mfano wa mshale
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtu mmoja, Musa Solela Ngasa (40), mkazi wa kijiji cha Nhobola kilichopo kata ya Tagala wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, amechomwa mshale kwenye ubavu upande wa kulia na watu wanane waliokuwa wakimshambulia kwa sababu ya mgogoro wa ardhi.
Tukio hili lilitokea Januari 21, 2025, saa 3 asubuhi, ambapo Musa alijeruhiwa kwa kuchomwa mshale kwenye mbavu ya mkono wa kulia.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa upelelezi bado unaendelea, huku mtuhumiwa mmoja akishikiliwa na wengine wakitafutwa.
Kwa upande wake, Ngasa ambaye hadi sasa yupo wodini akiendelea vizuri, amesema sababu ya kuchomwa na mshale inatokana na mgogoro wa eneo ambalo anamiliki kuhitajika na watu wengine, akieleza alifungua hadi kesi mahakamani kisha kushinda, lakini upande wa pili bado haujaridhika na maamuzi ya mahakama.
Musa Solela Ngasa ameeleza kwamba mgogoro huu wa ardhi umeendelea kwa miaka mitano, baada ya yeye kushinda kesi ya ardhi mahakamani, ambapo alipewa eneo lililokuwa likilalamikiwa na watu hao.
Amesema kuwa, siku ya tukio, alipokuwa akitoka shambani, alikutana na watu hao wanane ambao walimshambulia kwa mshale.
Ni mara ya nne kwa Musa kushambuliwa na watu hawa, ambapo awali walimpiga na kumjeruhi kwa panga na mara ya pili alijeruhiwa kichwani.
Ametoa shukrani za dhati kwa huduma aliyoipata kutokwa kwa Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga, akieleza ni nzuri na imesaidia kuokoa maisha yake.
Ndugu wa Musa, Magreth Ngasa, ameeleza jinsi alivyopata taarifa ya kaka yake kujeruhiwa, akisema kwamba alijua kuwa mgogoro wa ardhi ulikuwa unamsumbua ndugu yake kwa muda mrefu.
Daktari kutoka Idara ya Upasuaji, Matinde Joseph Dotto, ameeleza kuwa Mgasa alifikishwa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga majira ya asubuhi akiwa anavuja damu nyingi, kisha kufanyiwa huduma ya kwanza kisha kupelekwa chumba cha upasuaji.
Amesema kuwa jeraha na kuvuja kwa damu nyingi kulisababishwa na mshale uliomchoma na kuingia zaidi ndani, kiasi kilichopelekea hali yake kuwa kisha kufikishwa haraka hospitalini.
“Tulimpokea akiwa katika hali mbaya akiwa anavuja damu nyingi kisha tukampatia huduma ya kwanza.
“Tulifanikiwa kumfanyia upasuaji na kufanikiwa kuondoa kitu chenye ncha kali ambacho kilichoma hadi eneo la ini na sasa hali yake inaendelea kuimarika”, amesema Dkt. Matinde.
Social Plugin