Muonekano wa Barabara ya Kihamili Wilayani Mbinga
Mafundi wakiendelea na Ujenzi wa Barabara ya Kihamili Mbinga
Na Regina Ndumbaro - Mbinga Ruvuma.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, umetenga zaidi ya shilingi milioni 468 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kihamili-Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa barabara hiyo unalenga kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa kata ya Kigonsera na maeneo jirani.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga, Oscar Mussa, amesema barabara hiyo ina urefu wa kilomita 3.4 na inajengwa kwa awamu. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ujenzi wa kiwango cha lami umefikia mita 750. Uboreshaji huo unalenga kuwaondolea wananchi adha ya usafiri wanapokwenda kupata matibabu katika hospitali ya halmashauri pamoja na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo.
Mussa ameongeza kuwa, kazi nyingine muhimu zilizotekelezwa ni pamoja na kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilomita 3.5 kuelekea makazi mapya ya viongozi wa halmashauri. Pia, ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji eneo la mradi unaendelea, huku hatua za kuweka alama za barabarani na kufunga taa zikiwa zimetarajiwa kukamilishwa katika siku za karibuni.
Barabara hiyo pia itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Kigonsera, ambao walikuwa wakikumbana na changamoto za usafiri. Eneo la Kihamili, ambalo ni kioo cha kata ya Kigonsera, linatarajiwa kunufaika kwa kiwango kikubwa kupitia maboresho haya.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera, Benson Chiwinga, amesema miradi kama hii imeleta faida nyingi kwa vijana wa eneo hilo, wakiwemo waliopata ajira za muda na ujuzi wa kiufundi kupitia ujenzi wa barabara. Ameongeza kuwa, baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, vijana wanaweza kutumia maarifa yao kuendeleza maisha yao na kuepuka vitendo vya kihalifu.
“Tunaipongeza sana Serikali kwa kuleta miradi hii. Ni msaada mkubwa kwetu sisi tunaoishi vijijini, kwani miradi hii inaboresha maisha yetu na kukuza uchumi,” amesema Chiwinga.
Mkazi mwingine, Haji Mbawala, ameeleza kuwa hapo awali barabara ya Kihamili-Hospitali ilikuwa mbovu, hasa wakati wa mvua ambapo madimbwi mengi katikati ya barabara yalifanya shughuli za kilimo na usafiri kuwa ngumu.
Amesisitiza kuwa uboreshaji wa barabara hiyo utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
TARURA imeendelea kuwahimiza wakazi wa wilaya ya Mbinga kushirikiana kwa karibu na mamlaka hiyo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi. Lengo kuu ni kuboresha miundombinu ya usafiri na kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kiuchumi kupitia miradi kama huu.
Social Plugin