Na Regina Ndumbaro Mtwara.
Mkazi wa Nyasa, wilayani Masasi, mkoani Mtwara, maarufu kama Awilo, mwenye umri wa miaka 28, amekutwa amejinyonga ndani ya nyumba yake.
Tukio hili limetokea kwa mazingira ya kutatanisha, kwani Awilo hakukuacha ujumbe wowote, hali iliyoacha maswali mengi kwa familia, majirani na vyombo vya usalama.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyombo vya usalama, Jeshi la Polisi Wilaya ya Masasi lilipokea taarifa za tukio hili na mara moja walifika eneo la tukio.
Polisi walilazimika kuvunja mlango wa nyumba ya marehemu, ambapo walikuta mwili wa Awilo ukiwa umening'inia, jambo lililowaacha majirani na familia katika hali ya kutoelewa kilichosababisha tukio hilo.
Madaktari kutoka Hospitali ya Mkomaindo wamefika eneo la tukio na kuthibitisha kifo cha Awilo.
Mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo, na uchunguzi wa awali umeanza ili kubaini chanzo cha tukio hili la kusikitisha.
Diwani wa Kata ya Nyasa, Mbaraka Kodo, amefika eneo la tukio na kugundua kuwa marehemu ni ndugu yake wa karibu. Hali hiyo imemwacha katika mshangao na huzuni kubwa, huku akitoa pole kwa familia na majirani waliokusanyika kushuhudia tukio hilo.
Kwa upande wa majirani, wameelezea mshtuko wao na kusema kuwa Awilo alikuwa kijana mwenye tabia njema na mpenda amani. Wamesema hawakuwahi kuona dalili zozote za changamoto za kiakili au kihisia kwa marehemu, na hivyo tukio hili limetokea kwa ghafla na kutoeleweka.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa kesho, tarehe 19 Januari,2025.
Tukio hili linawaacha wengi wakiwa na maswali kuhusu chanzo cha kifo cha kijana huyo, huku familia na jamii ya Nyasa wakiwa katika majonzi makubwa. Uchunguzi wa polisi unaendelea ili kubaini sababu kamili ya kifo hicho.
Social Plugin