Emmanuel Ntobi
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Kamati Tendaji ya CHADEMA Kanda ya Serengeti imemvua uenyekiti Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, kufuatia tuhuma za kimaadili alizokuwa akituhumiwa nazo.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha kawaida cha kamati kilichofanyika Januari 8, 2025, mjini Shinyanga, ambapo Ntobi alipewa nafasi ya kujitetea mbele ya kamati.
Katibu wa Kamati Tendaji ya Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawi, amesema kamati ilifikia uamuzi wa kumvua Ntobi nafasi yake ya uongozi baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na kwa kauli moja.
“Hivyo tunapenda kuujulisha umma kuwa kuanzia sasa, Mhe. Emmanuel Ntobi siyo mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga,” amesema Mnyawi.
Kwa upande wake, Emmanuel Ntobi amekataa tuhuma dhidi yake na kusema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya "joto la kisiasa" kutokana na msimamo wake wa kumuunga mkono Freeman Mbowe, anayewania nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Ntobi amesema hatua hiyo ni "ajali ya kisiasa" inayotengenezwa na wafuasi wa Tundu Lissu, ambao kwa madai yake ni baadhi ya viongozi wameungana kumchukulia hatua kinyume cha taratibu.
"Sijapelekwa kwenye kamati ya maadili, hili ni joto kubwa la kisiasa kufuatia uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, nimeonewa kwa sababu ya joto la kisiasa" amesema Ntobi.
Hadi sasa, uamuzi wa kumvua Ntobi uenyekiti umeibua masuala ya kiutawala na kisiasa ndani ya chama, huku mchakato wa uchaguzi wa uongozi wa CHADEMA Taifa ukitarajiwa kuleta mabadiliko zaidi katika chama hicho.
Social Plugin