Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. MAYALA ATOA MUAROBAINI WA KUYAEPUKA MAGONJWA HATARI

 


Ahimiza utumiaji wa vyakula vya asili

Na Lydia Lugakila - Bukoba

Jamii Mkoani Kagera imehimizwa kutumia vyakula vya asili ili kuepuka magonjwa mbalimbali yakiwemo yanayojitokeza kwa wingi kwa nyakati hizi.

Kauli hiyo imetolewa na Dk. John Mayala kutoka zahanati ya St. John iliyopo Manispaa ya  Bukoba Mkoani Kagera wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.

Dkt. Mayala amesema kuwa jamii ya sasa imepuuza kutumia vyakula vya asili hali iliyosababisha mtu kupata magonjwa mbali mbali yakiwemo ya sukari, maumivu ya viungo kansa, presha na mengine mengi.

Amesema kuwa mwili wa Binadamu unajengwa na seli mbali mbali ambapo kila seli ina kazi yake na kuwa kila seli utengeneza kitu kiitwacho Radicals ambao ni uchafu unaotengenezwa kwenye seli.

Amesema kuwa Radicals nyingi zinatengenezwa kutokana na kutokutumia vyakula vya asili ikiwemo karoti, mboga za majani, matunda kwani hivyo ni vyakula muhimu  katika kujenga mwili ambapo pia ameongeza kuwa miili ya mwanadamu inashambuliwa sana na magonjwa huku tatizo likiwa ni kupuuza vyakula vya asili.

"Radicals zinapokuwa nyingi katika mwili wa binadamu zina madhara zikibadilika ndo maana  mtu hupata maumivu kama ya kuchomwa chomwa na vitu mwilini hivyo mwili unahitaji Anti- oxidants ambazo ni kemikali zinazozalishwa sehemu mbali mbali za mwili na kazi yake ni kuondoa sumu mwilini" amesema Dkt. Mayala.

Aliongeza kuwa ubichi wa vyakula ikiwemo kabichi, nyanya, vitunguu, karoti na vinginevyo vyenye kujenga mwili vina utajiri mkubwa wa kutengeneza mwili vizuri kuliko vilivyopikwa kwani vya kupikwa vinakuwa tayari vimepoteza virutubisho muhimu.

Dkt. Mayala amevitaja vyakula vilivyobeba Anti-oxidant kwa wingi kuwa ni vya vitamini A-C-E na D kwani husaidia kuleta Anti-oxidant mwilini.

Amesema vitamini A inabeba karoti kwa wingi mboga za majani, mayai matango,tikitimaji na parachichi na C- hubeba matunda yakiwemo tufaa, nanasi, limao na E hubeba karanga, machungwa, nyanya, mafuta ya mmea, machenza, maembe, papai na mboga za majani.

Aidha Amesema radicals zinapokuwa nyingi  mwilini huleta madhara ikiwemo kansa, kusababisha kuzeeka haraka kabla ya umri, magonjwa ya ngozi huku akiongeza kuwa wavutaji wa sigara wanatengeneza Radicals nyingi mwili mwao na hawajui kuwa sigara ni chanzo cha kansa.


Ameongeza kuwa pia watumiaji wa pombe kali aina ya spirits nao wanatengeneza Radicals kwa wingi, na mtu anapougua, kuvuta hewa chafu, kula mafuta mengi husababisha uwepo wa Radicals nyingi mwilini.


Hata hivyo aliitaka jamii Mkoani Kagera kuendeleza vyakula vya asili ili kujiepusha na magonjwa yanayowagharimu kiasi kikubwa cha fedha huku akiwahimiza kupima Afya zao inapobidi ili kuyaepuka magonjwa mbali mbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com