Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI MBIONI KUINGIA MKATABA WA SGR KUTOKA KIGOMA HADI BURUNDI




Na Mwandishi Wetu, KIGOMA.

SERIKALI inatarajia kuingia mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Bujumbura nchini Burundi ambapo badaye kuendelezwa kutoka Bujumbura hadi Kindu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameyasema hayo jana alipotembelea kipande cha sita cha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilometa 506, mradi unaogharimu kiasi cha sh. trilioni 6.3 huku mradi huo ukitarajiwa kukamilika Machi 2027.

“Wale wanaosema Kigoma ni mwisho wa reli, miaka miwili au mitatu ijayo hilo jambo litabadilika na Kigoma sasa itakuwa ni katikati ya reli,” amesema Mbarawa.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na kero mbalimbali ambazo mkandarasi amezieleza lakini waatalamu wapo na wanazifanyia kazi, ambazo nyingi ni za kihandisi na kuwahakikishia wananchi kuwa kazi hiyo itakwenda kwa kasi inayotakiwa.

Meneja wa mradi huo Mhandisi Wallace Isaya amesema kuwa ujenzi huo umekuwa na kero katika eneo la mto Maragarasi kutokana na mvua nyingi ambazo huleta athari kwa kipindi cha takribani miezi saba kila mwaka.

"Lakini pia pamoja na kuwepo na kero hiyo, katika msimu wa kiangazi uliopita, mkandarasi amefanikiwa kujenga nguzo 13 za daraja hili, amebainisha Mhandisi Isaya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani amesema kuwa Kigoma ilikuwa inaonekana iko mbali lakini kwa miradi kama hiyo haitakuwa mbali tena kwani wananchi wataweza kusafiri kwa urahisi mara itakapokuwa imekamilika.

Pia Mathamani ameishukuru serikali kwa uwekezaji huo na kuufungua mkoa wa Kigoma huku akibainisha kuwa miradi hiyo italeta fursa za kiuchumi kwa wananchi kwani wawekezaji wengi watafika mkoani humo kutokana na ardhi yao kuwa ni yenye rutuba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com