Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM SONGEA MJINI YAIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA FEDHA ZA MRADI WA MAJI WA MIJI 28

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea Mwinyi Msolomoni(katikati) )kulia kwake ni James Mgego Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea mjini na kushoto kwake ni Mhandisi Vincent Bahemana ambaye ni msimamizi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

 



Na Regina Ndumbaro Ruvuma 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini kimempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi bilioni 145.77 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma. 


Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mwinyi Msolomi, wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya siasa waliotembelea mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).


Msolomi amesema mradi huo ni muhimu kwani unatarajiwa kumaliza changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali, hususan mtaa wa Sokoine na kata ya Making’inda.


 Ameongeza kuwa mradi huo utaimarisha maisha ya wananchi kwa kuwaondolea adha ya kutafuta maji kwa muda mrefu na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.


Katibu wa CCM wilaya ya Songea, James Mgego, ameitaka Serikali kutoa fedha zilizobaki ili kuhakikisha mkandarasi anaendelea na ujenzi wa mradi huo ambao ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha.


 Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika kwa zaidi ya miaka 20.


 Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Vicent Bahemana, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Januari 2024 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2026. 


Amefafanua kuwa Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni 21.87 kama malipo ya awali kwa mkandarasi, huku kazi mbalimbali zikiendelea kufanyika, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba.


Mradi huo unahusisha ujenzi wa kidaka maji katika Mto Njuga chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 17 kwa siku, mtambo wa kuchuja na kutibu maji lita milioni 16, na matenki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9.


 Pia, unahusisha upanuzi wa mtandao wa mabomba ya maji na ukarabati wa mtambo wa kuchuja maji wenye ufanisi wa chini ili kukidhi mahitaji ya Manispaa ya Songea.


Msolomi na wajumbe wengine wa kamati ya siasa wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo lakini wameitaka Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji. 


Pascal Msigwa, mjumbe wa kamati hiyo, ameitaka Serikali kuharakisha mradi huo ili kuwasaidia wananchi kuondokana na mgao wa maji.


Kwa sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 4.8, huku matenki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 kila moja yakikamilika, na ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 5 ukiwa katika hatua za msingi. 


Serikali inatarajiwa kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa ufanisi ili kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Songea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com