Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YASHAURI KUPANULIWA KWA MTANDAO WA GESI ASILIA KWA MIKOA YA NJE YA DAR ES SALAAM


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuongeza ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari katika maeneo ya mikoani ili kuchochea matumizi ya gesi katika vyombo vya moto.

Ushauri huo umetolewa leo Januari 25, 2025 wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha kushindilia gesi asilia (CNG) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam .

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, David Mathayo amesema kuna haja ya serikali kujenga mabomba ya gesi kuelekea mikoani badala ya kutegemea malori kusafirisha gesi.

“Kupanua mabomba ya gesi hadi mikoa mingine kutawafaidi wamiliki wa magari kote nchini na kuleta upatikanaji wa nishati nafuu na endelevu,” Amesema Mathayo.

Aidha Kamati hiyo iliainisha wasiwasi kuhusu makubaliano kati ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na TPDC kuhusu ardhi iliyotengwa kwa ajili ya kituo kikuu cha CNG. Kwa sasa Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) inakodi ardhi hiyo kutoka Chuo, lakini kamati imeshauri TPDC ipatiwe ardhi hiyo bure.

“Kwa kuwa taasisi zote hizi ni za umma zinazohudumia raia, kuondoa mkataba wa kodi kutapunguza gharama za uendeshaji na hivyo kupunguza bei kwa watumiaji,” Amesema Mwenyekiti wa Kamati Mathayo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kubuni mazingira rafiki kwa uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya CNG.

Amesema kushirikiana na sekta binafsi, serikali inatarajia kuharakisha maendeleo ya mtandao wa CNG kote nchini.

Pamoja na hayo amesema kuwa kubadili matumizi ya CNG kama nishati ya usafiri kuna faida kubwa kiuchumi na kimazingira.

Amesema kuwa CNG ni mbadala nafuu na safi kwa dizeli na petroli, inapunguza utoaji wa gesi chafu na uchafuzi wa hewa katika maeneo ya mijini.

Aidha, amesema kutumia gesi asilia inayozalishwa nchini kunapunguza utegemezi wa nchi kwa mafuta ya kuagiza, na hivyo kuimarisha usalama wa nishati na kuokoa fedha za kigeni.

Nae Mkurugenzi wa Mpango na Uwekezaji wa TPDC, Derrick Moshi amesema kituo hicho kitachochea sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya CNG na kuvutia magari zaidi kutumia CNG badala ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo amesema Kituo hicho kitakuwa ni kituo cha kusambaza gesi kwa vituo vidogo, kitasaidia kupunguza msongamano na kufanya gesi asilia kupatikana kwa urahisi zaidi.

Amesema vituo vingine vidogo vya Muhimbili na Kibaha vitapanua huduma katika maeneo muhimu na kupunguza umbali wa safari kwa watumiaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com