Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAAFISA UGANI 91 KUPATA AJIRA MTWARA


Na Regina Ndumbaro Mtwara.

Maafisa ugani wapatao 91 wanatarajiwa kuanza ajira za muda mfupi katika mkoa wa Mtwara, wakihudumu wilayani Masasi na Nanyumbu. 

Afisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Korosho, Ndugu Geofrey, amesema kuwa maafisa hao wanashiriki semina ya siku tano inayoendeshwa na bodi hiyo ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Katika semina hiyo, maafisa ugani hao wameelezwa kuwa watapatiwa pikipiki na vishikwambi vitakavyorahisisha utendaji wao wa kazi mashambani. 

Pia, wametakiwa kushirikiana na wakulima kutatua changamoto zao za kilimo, kufufua mashamba yasiyotumika, na kuongeza uzalishaji wa mazao hasa korosho kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo.

Maafisa ugani hao wamepewa mafunzo kuhusu maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wakulima. Mafunzo hayo yameratibiwa na wawezeshaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania na yanaendelea katika mikoa mingine ikiwemo Lindi, Ruvuma, na Pwani, ambako vijana takribani 500 watafaidika na ajira hizi za muda mfupi.

Katibu Tarafa wa Wilaya ya Masasi, Ndugu Fikiri Lukanga, amefungua semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Ndugu Lauter John Kanoni. Katika hotuba yake, amewataka maafisa ugani kufuata maadili ya kazi, kujiepusha na rushwa, na kushirikiana na maafisa kilimo waliopo katika maeneo yao ya kazi.

Ndugu Lukanga amesisitiza kuwa ni muhimu maafisa hao kutumia muda mwingi mashambani kusaidia wakulima, hasa katika kipindi hiki muhimu cha msimu wa kilimo. Amesema ushirikiano wao na wakulima ni kiini cha kufanikisha malengo ya uzalishaji wa korosho katika mkoa wa Mtwara.

Kwa upande wao, maafisa ugani wamesema wako tayari kufanya kazi katika maeneo watakayopangiwa na kuahidi kushirikiana na wakulima kwa bidii ili kufanikisha malengo ya serikali ya kufikia uzalishaji wa tani 700,000 za korosho msimu wa 2025/26 na tani milioni moja msimu wa 2026/27.

Ajira hizi za muda mfupi zinatarajiwa kuchochea uzalishaji wa korosho na kuinua uchumi wa wakulima wa mkoa wa Mtwara, ambao ni moja ya mikoa kinara wa uzalishaji wa zao hilo nchini Tanzania.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com