Na Regina Ndumbaro - Ruvuma
Diwani wa Kata ya Misufini B, Manispaa ya Songea Mjini, mkoani Ruvuma, Christopher Fabian Kayombo leo tarehe 8 Januari, 2025 amekabidhi madawati 135 kwa Shule ya Msingi Misufini ili kuboresha mazingira ya kujifunzia wanafunzi.
Tukio hilo limefanyika kwa ushirikiano wa karibu na Mratibu wa Kata, Ndugu Adolf Challe, ambapo madawati hayo yamekabidhiwa rasmi kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ndugu Credo Komba, pamoja na Mtendaji wa Mtaa, Bi Agnes Ndunguru.
Diwani Kayombo amesema kuwa wanaishukuru serikali ya mama samia kwa na mkurugenz wa Manispaa Ya songea kwa kuwapa kiasi cha fedha shilingi milioni 25 kwa ajili ya madawati na pia ametoa kiasi cha shilingi milioni 13 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa katika shule hiyo.
Katika ukabidhi huo wa madawati viongozi waliohudhuria ni pamoja na Katibu mwenezi wa Kata wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Misufini B, pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Misufini, Bi Bahati Ally Mbano.
Wakati wa makabidhiano hayo, Diwani huyo amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na jamii ili kuimarisha sekta ya elimu, huku amewataka wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono jitihada za maendeleo ya shule.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ndugu Credo Komba, amewashukuru viongozi wa serikali na wadau wote waliosaidia kufanikisha upatikanaji wa madawati hayo.
Amesema kuwa madawati hayo yamekuja wakati muafaka, kwani shule hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati, hali iliyokuwa ikihatarisha ubora wa elimu.
Naye Mtendaji wa Mtaa, bi. Agnes Ndunguru, ametoa pongezi kwa Diwani na viongozi wote waliounga mkono juhudi hizo huku amesema kuwa hatua hiyo ni mfano wa uongozi bora na wenye kujali maendeleo ya wananchi pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kuboresha miundombinu ya shule ili kuinua viwango vya elimu katika eneo hilo.
Kwa upande wake Mratibu Kata kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Adolf Challe, amewahimiza wananchi wa Misufini B kuendeleza mshikamano na kushirikiana na viongozi wao katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema kwamba wamejipanga vyema na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha maendeleo ya wanafunzi katika sekta ya elimu.
Social Plugin