Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea wakiwa katika Bustani za Msitu huo ya Matogoro
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanal Ahmed Abbas katikati Mkuu wa Wilaya ya Songea Mjini Kapenjama Ndile na Kushoto ni Mhifadhi wa Msitu Asili wa Matogoro Musa Kitivo
Na Regina Ndumbaro Ruvuma.
Jumla ya watalii 871 wa ndani na 9 kutoka mataifa ya kigeni wametembelea msitu wa hifadhi ya asili wa Matogoro uliopo kata ya Ndilimalitembo, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, na kuchangia zaidi ya shilingi 1,472,390 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Mhifadhi wa Msitu huo, Mussa Kitivo, alipokuwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, aliyetembelea msitu huo jana.
Kwa mujibu wa Kitivo, mwaka wa fedha 2023/2024 uliwashuhudia watalii 2,341 wa ndani na 30 wa nje wakitembelea msitu huo, huku mapato ya shilingi 5,467,000 yakikusanywa kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Amebainisha kuwa mwaka 2021/2022 TFS ilipokea shilingi 394,135,000 kutoka mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya vumbi yenye urefu wa kilometa 9.
Kitivo ameeleza kuwa kazi nyingine zilizokamilika ni ujenzi wa njia ndogo ya miguu yenye urefu wa kilometa 4.3, kuboresha lango kuu la kuingia msituni, na kuimarisha vivutio mbalimbali. Vivutio hivyo ni pamoja na miinuko mikubwa inayotoa mwonekano mzuri wa mji wa Songea na vijiji vyake, chanzo cha Mto Ruvuma wenye urefu wa kilometa 800, na vyanzo vingine vya maji vinavyotegemewa na wakazi wa Songea kwa matumizi ya kila siku.
“Msitu wa Matogoro una vivutio vya kipekee, ikiwemo mapango yanayotumika kwa tiba za jadi na matambiko, pamoja na wanyama kama swala, digidigi, nyani, simba, na ndege mbalimbali. Aidha, hali ya hewa ya msitu huu ni tofauti na maeneo mengine ndani ya Ruvuma,” amesema Kitivo.
Kitivo ameongeza kuwa mkakati wa TFS kwa sasa ni kutafuta mwekezaji atakayejenga hoteli ya kitalii kwenye eneo la milima (viewpoint), kuongeza idadi ya watalii kufikia 5,000 mwaka huu, na kuboresha miundombinu ya msitu kwa kuweka choo cha kudumu, jiko la kisasa, na vifaa vya michezo kwa watoto. Pia, TFS inapanga kuanzisha utalii wa kuruka na parachuti kutoka viewpoint ya pili.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, amewapongeza wakala wa TFS kwa juhudi kubwa katika uhifadhi wa msitu wa Matogoro na vivutio vingine vya utalii mkoani humo. Ametoa wito kwa wakazi wa Ruvuma na kanda ya kusini kwa ujumla kutembelea vivutio vya utalii ili kujifunza na kuhamasisha uchumi wa ndani.
Kwa upande wake, Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini, Manyise Mpokigwa, amesema Ruvuma ina misitu minne ya asili inayotumika kwa utalii, ikiwemo msitu wa Mwambesi wilayani Tunduru. Amebainisha kuwa Matogoro pia una utalii mpya wa ikolojia ambao umeanza kuvutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ndilimalitembo, Magnus Nyoni, amesema tangu msitu huo ulipohifadhiwa rasmi, wananchi wamefaidika kwa ajira, kuuza bidhaa kwa watalii, na kuongeza fursa za kipato. Ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuimarisha hifadhi hiyo, akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TFS katika kulinda urithi huo wa asili.
Social Plugin