Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KITANDULA ATOA WITO TANAPA KUITUNZA MIRADI YA REGROW MIKUMI


Zainab Ally – MIKUMI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, leo Januari 9, 2024, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania REGROW katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kitandula amekagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Kiwanja cha Kisasa cha Ndege, majengo ya kupokelea wageni, mageti mawili ya kisasa, na nyumba za kisasa za kupumzikia wageni.

Mhe. Kitandula amewataka wasimamizi wa mradi huo kutunza miundombinu ya kisasa inayojengwa, akisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa miradi hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuboresha huduma kwa wageni, na kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi ya Taifa Mikumi, jambo litakaloongeza mapato ya utalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya jirani.

“Miundombinu hii ya kisasa ni muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi na kijamii, hususan kwa jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa Mikumi, tunahitaji kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na fursa zinazotokana na mradi huu,” alisema Mhe. Kitandula.

Mradi wa REGROW, unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania, unalenga kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha usimamizi wa maliasili, na kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii. Kupitia mradi huo, maeneo muhimu ya Hifadhi ya Mikumi yameboreshwa, yakiwemo miundombinu ya barabara, vituo vya taarifa, na huduma bora za wageni. Mhe. Kitandula alisisitiza umuhimu wa miradi hii katika kuimarisha sekta ya utalii, huku akiwataka wasimamizi kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuisimamia vyema na kuitunza miundombinu hiyo.

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki John Nyamhanga, alieleza jinsi mradi wa REGROW ulivyobadilisha muonekano wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, huku akikazia namna uboreshaji wa miundombinu hiyo utaongeza mazao ya utalii, hivyo kuhamasisha ongezeko la idadi ya watalii na kukuza pato la Taifa.

Mradi wa REGROW katika hifadhi ya Taifa Mikumi ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kutunza na kuendeleza rasilimali za asili za nchi kwa ajili ya manufaa ya wananchi na ustawi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com