Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kanali Ahmed Abbas akizindua kampeni ya mpango harakishi wa uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro Ruvuma.
Kampeni hii imezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, katika viwanja vya Soko Kuu la Manispaa ya Songea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika tarehe 23 mwezi wa kwanza 2025 Kanali Abbas amebainisha kuwa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa tisa nchini ambayo ilibua wagonjwa wachache wa kifua kikuu mwaka 2024, kwa kufikia wagonjwa 1,278 tu, sawa na asilimia 50.78 ya lengo la wagonjwa 2,515.
Ameongeza kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwaka 2024 kulikuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu milioni 10.8 duniani kote, huku milioni 1.25 wakiwa wamefariki dunia.
Kwa upande wa Tanzania, Kanali Abbas amesema kuwa wagonjwa wapya wa kifua kikuu wanakadiriwa kufikia 122,000 sawa na wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000, huku walioibuliwa na kuanzishiwa matibabu wakiwa asilimia 76.
Katika mkoa wa Ruvuma, asilimia ya wagonjwa walioibuliwa ni 50.79, na hivyo kuna changamoto ya kuwafikia wagonjwa 1,132 waliobaki ambao bado wanaweza kuambukiza jamii.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa serikali imechukua hatua madhubuti kupambana na ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja na kuongeza mashine saba za kugundua vimelea vya kifua kikuu katika hospitali na vituo vya afya vya mkoa wa Ruvuma. Mashine hizo zimefungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga, na vituo vya afya vya Mjimwema na Mkiri, kati ya vingine.
Kampeni hii itatekelezwa katika halmashauri saba za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Manispaa ya Songea, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Nyasa, Mbinga, Namtumbo, Tunduru, na Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Mkuu wa Mkoa amehimiza viongozi wa wilaya kuhakikisha wanahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya afya ili kuchunguzwa na kupatiwa matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Chihoma Mhako, ameeleza kuwa juhudi za uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu zinaendelea kupitia watoa huduma ngazi ya jamii. Aidha, amesema kuwa mkoa wa Ruvuma unaendelea kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu kwa kushirikiana na wizara ya afya ili kufanikisha kampeni hii na kuokoa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dkt. Jackob Mwanamtwa, amesema kuwa kampeni hii inalenga kuwafikia wananchi ambao hawakufikiwa na huduma za uchunguzi na matibabu kwa mwaka 2024, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kupunguza maambukizi ya kifua kikuu.
Social Plugin