Habari Mpya

    Loading......

MKUU WA WILAYA YA MASASI ASISITIZA WATUMISHI KUTIMIZA MAJUKUMU YAO KWA KUEPUKA VITENDO VYA KIBAGUZI KWA WANANCHI




Na Dotto Kwilasa, Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Luteni John Kanoni, amewataka watumishi wa wilaya hiyo kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kujiepusha na vitendo vya kubagua, kuchelewesha huduma, au kuwa chanzo cha kero kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa ni jukumu la kila mtumishi wa umma kuhakikisha anatoa huduma bora, kwa wakati, na kwa usawa kwa wananchi, kwani hiyo ni haki ya kisheria ya kila raia.

Hayo yamesemwa na Luteni Kanoni, Januari 30, 2025, wakati wa Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora kwa viongozi, ambayo yanaendelea kutolewa mkoani Mtwara na Wizara ya Katiba na Sheria.

Mafunzo haya yanafanyika kwa sasa katika Halmashauri ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, na yanapata umaarufu mkubwa kutokana na umuhimu wake katika kuboresha utendaji mkoani hapo
Aidha mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba viongozi na watumishi wa umma wanapata uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za raia.

Akizungumza kwenye ,mafunzo hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Masasi amesema yanasaidia kuwaongezea viongozi uwezo wa kushughulikia matatizo ya wananchi kwa njia ya haki, uwazi, na ufanisi.

Luteni Kanoni pia amewaambia viongozi na watumishi wa wilaya hiyo kuwa, ili kufanikisha maendeleo endelevu katika jamii, ni lazima huduma zote zitolewe kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

Amewataka viongozi kuwa mfano bora katika jamii na kuepuka tabia zinazoweza kuleta mgawanyiko au kukwamisha maendeleo.

"Utawala bora haueleweki tu kwa maneno, bali pia kwa matendo ya kila siku ya viongozi na watumishi wa umma," amesema Luteni Kanoni.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wameametoa shukrani kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo haya muhimu kwa viongozi na watumishi wa wilaya.

Lilian galahenga Mtendaji wa kata ya Nanyumbu amesema kuwa mafunzo haya yataongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuboresha uhusiano kati ya Serikali na wananchi, hivyo kuchochea maendeleo katika wilaya hiyo.

Ameongeza kwamba, kupitia mafunzo hayo, viongozi wataweza kuelewa umuhimu wa kushirikiana na wananchi katika kufanya maamuzi ambayo yana manufaa kwa jamii nzima.

Naye Fatma shidoli Kaimu mtendaji Kata ya Namajani amesema elimu ya uraia ni sehemu muhimu ya kuimarisha demokrasia na utawala bora ambapo wao kwa nafasi yao wataenda kuwanufaisha wananchi kwa kuwapa elimu hiyo ili kuwawezesha kuelewa haki zao na wajibu wao katika jamii.

"Hivyo, ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa umma kuelewa kuwa utawala bora haujengi tu ufanisi wa serikali, bali pia unahamasisha ushirikiano na amani katika jamii, " Amesema
Amesema katika muktadha huo wananchi wanakuwa na haki ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya kimaamuzi na maendeleo yanayowahusu, huku wakilindwa na Serikali kutoka kwa vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji.

Mafunzo haya, yakiwa na lengo la kuboresha utendaji kazi katika serikali za mitaa, ni muhimu katika kuhakikisha kwamba kila raia anapata huduma za msingi kwa usawa na kwa haki.

Pamoja na mambo mengine Lengo kuu la mafunzo haya ni kutoa elimu kuhusu haki za kiraia, majukumu ya viongozi na watumishi wa umma, na namna ya kusimamia utawala bora kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com