Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTWALE ASISITIZA UBUNIFU KATIKA KUANDAA NA KUTEKELEZA MIPANGO YA KUKUZA UCHUMI NCHINI



Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kuwa wabunifu katika kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi inayolenga kutatua changamoto za uchumi na uzalishaji katika mikoa na halmashauri wanazozisimamia.

Bw. Mtwale wito huo leo katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mipango ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 pamoja na kuandaa mipango ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

“Sehemu za uchumi na uzalishaji katika mikoa ndio zinabeba dira ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu katika nchi yetu hivyo ni muhimu mipango yenu ilenge vipaumbele vya Serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa uchumi mahalia,” Bw. Mtwale amesisitiza.

Bw. Mtwale amehimiza kuwa, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na maandalizi ya Mipango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ni vema mipango na bajeti za mikoa na halmashauri zikazingatia mwongozo wa bajeti na vipaumbele vya nchi ili kuakisi utatuzi wa matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wananchi na taifa kwa ujumla.

Sanjari na hilo, amewakumbusha Makatibu Tawala hao Wasaidizi wa Mikoa kuwa, wanajukumu muhimu katika maendeleo ya taifa hivyo waendelee kutekeleza majukumu yako kwa weledi na uzito unaostahili ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao hususani katika kutatua changamoto za uchumi na uzalishaji kwenye mikoa na halmashauri wanazozisimamia.

Kwa upande wake, mwakilishi wa makatibu tawala hao wasaidizi Bw. Said Maditto ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya amesema kuwa kitendo cha kufanya kikao kazi na wakurugenzi wa wizara za kisekta ni fursa ya kujenga ushirikiano wa kiutendaji katika kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi nchini.

Aidha, Bw. Maditto amemuahidi Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale kuwa watatekeleza kwa vitendo maelekezo yote aliyoyatoa pamoja na kutekeleza maazimio wakakayotokanayo katika kikao kazi hicho kwa lengo la kuandaa mikakati na mipango endelevu itakayokuza uchumi wa taifa.

Naye, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta amesema TAMISEMI iliona ni muhimu kukutana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji pamoja na wakurugenzi wa Wizara za Kisekta kwa ajili ya kupata maoni, maono na mtazamo wa namna bora ya kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi nchini.

Pia, Bi. Kimoleta ameongeza kuwa kikao kazi hicho kitatoa fursa ya kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuona nini kimetekelezwa mpaka hivi sasa na ni changamoto zipi zifanyiwe kazi ili zisikwamishe utekelezaji wa bajeti hiyo.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimeudhuriwa na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kutoka mikoa 26, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Wizara za Kisekta pamoja na Wakurugenzi na Wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com