Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENYEKITI JUMUIYA YA WAZAZI MKOA WA DSM AENDELEA KUTOA MSAADA KWA KAYA ZENYE UHITAJI MAALUMU


January 8,2025

Mwenyekiti wa wazazi, Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Khadija Ally Said, ameendelea kutimiza ahadi yake ya kugawa viti mwendo kwa watu wenye mahitaji maalum, na safari hii amezifikia kaya tano za kata ya mjimwema, wilaya ya Kigamboni.

Akiambatana na Diwani wa kata hiyo, Mheshimiwa Omary Ngurangwa, mwenyekiti wa wazazi, wilaya kigamboni, Greyson Mwikola na viongozi wengine wa chama na Serikali akiwemo Afisa Ustawi wa jamii kata ya Mjimwema, Watendaji wa mitaa yote minne, na viongozi wa Chama ngazi ya kata, amefanikiwa kutembelea wahitaji kutoka kaya tano na kuwapatia viti mwendo.

"Leo tuko hapa Mjimwema ikiwa ni juhudi zetu kama jumuiya ya wazazi kurejesha kwa jamii na kuwapa matumaini na faraja ndugu zetu hawa wenye uhitaji maalum." Amesema Bi. Khadija

Zoezi la kugawa viti mwendo ni sehemu ya mchango wa Mwenyekiti wa Wazazi, Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Khadija Ally Said ambapo hadi sasa ameshagawa zaidi viti mwendo 55 kwa familia zenye watu wenye mahitaji maalum katika mkoa wa DSM.

Akishukuru kwa niaba ya Serikali, Afisa Ustawi wa Jamii, kata ya Mjimwema, Bwana Dodo amesema kata hiyo iko na watu 20 wenye mahitaji ya viti mwendo, na mchango uliotolea utasaidia kupunguza idadi ya wahitaji na kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa Bi. Khadija Ally Said.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com