Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,ameonyesha kukasirishwa na kitendo cha wananchi wa kijiji cha Mwang'halanga kuchangishwa fedha za kupaua jengo la Zahanati ya kijiji hicho sh.milioni 11.7 lakini fedha hizo zimeshindwa kutekeleza ujenzi huo.
Mtatiro amesikitishwa na kitendo hilo leo Januari 15,2025 wakati akisikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Mwang'halanga na kuzitatua,ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake kufikia kila kijiji kusikiliza kero za wananchi,ambapo amefika pia kijiji cha Singita na Manyada.
Amesema kwa changamoto ya wananchi wa kijiji cha Mwang'halanga kushindwa kupauliwa Zahanati yao, na wakati wamechangishwa fedha kila Kaya Sh.28,000, na kuna Kaya 418 sawa na sh.milioni 11.7, lakini fedha hizo hadi leo hazijapaua jengo hilo la Zahanati,na kwamba huko ni kucheza na pesa za wananchi.
"Acheni mchezo na pesa za wananchi,dunia gani utapata wananchi wanachangishana fedha hadi Sh.milioni 11 utawapata wapi,leo mnakuja kuniambia zimekwama kwenye mfumo wa NeST hili hapana," amesema Mtatiro.
"Haiwezekani Mtendaji wa Kijijji amechangisha pesa wananchi, na pesa hizo akaziweka kwenye Akaunti ya kijiji kwa uaminifu kabisa pamoja na fedha za mfuko wa jimbo Sh.milioni 3 jumla milioni 14,na hadi sasa jengo hilo halijapauliwa,na kunieleza sababu ni mfumo wa NesT huku ni kucheza na pesa za wananchi,"ameongeza Mtatiro.
Aidha,ameagiza Menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,kwamba ifikapo tarehe 27/1/2025 kuwa siku hiyo ni siku ya kwenda kupaua jengo la Zahanati hiyo, na yeye atafika hapo pamoja na Kamati yake ya ulinzi na usalama kupaua pamoja na wananchi.
Mtendaji wa kijiji cha Mwang'halanga Helena Kayagila,amesema wananchi wa kijiji hicho walichangishwa fedha hizo Agosti 30 mwaka jana,pamoja kutolewa sh.milioni 3 fedha za mfuko wa jimbo,na yeye akaziweka kwenye akaunti ya kijiji jumla sh.milioni 14.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu,akitoa majibu amesema kwamba upauaji wa jengo la Zahanati hiyo, limekwamishwa na tatizo la
mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma NeST.
Diwani wa Samuye John Ngengeshi,naye akizungumza kwenye mkutano huo, alikazia kwamba ukwamishaji wa fedha hizo za wananchi kupauwa zahanati ya kijiji hicho, linatokana na kukwama kwa mfumo wa NeST, sababu ambayo mkuu wa wilaya hakukubaliana nayo.
Nao baadhi ya wanakijiji cha Mwang'halanga akiwamo Manase Elias,awali walisema kama pesa zao walizochanga zimeshindwa kupaua Zahanati yao, ni vyema wakarudishiwa pesa hizo, na kwamba wao walilidhia kuchangishana ili wapate huduma za matibabu karibu na makazi yao lakini wanaona hakuna kinachoendelea.
Katika ziara hiyo ya Mkuu wa wilaya amesikiliza kero za wananchi ikiwamo changamoto ya ukosefu wa maji,ubovu wa miundombinu ya barabara,kutokamilika maboma ya zahanati,umeme,pamoja na migogoro ya ardhi,huku akiagiza wazazi kupeleka watoto wao shule, na kwamba mwisho itakuwa ijumaa na baada ya hapo zoezi la ukamataji lita anza.
TAZAMA PICHA 👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Usanda Edson Jisena akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Usanda Forest Nkole akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Samuye John Ngengeshi akizungumza kwenye mkutano huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu akitoa majibu kwenye mkutano.
Social Plugin