Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Serikali imesema licha ya elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria,bado kuna changamoto za uelewa wa kisheria katika jamii ikiwemo kwenye ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi, ndoa na ardhi.
Waziri wa Katiba na Sheria,Dk Damas Ndumbaro ameeleza hayo Jijini Dodoma leo January 20,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aids Compain (MSLAC) mikoa Sita itafikiwa kwa ajili ya uelimishaji.
Amesema kupitia MSLAC wamebaini kuwa kwenye sekta ya ardhi kuna ubabaishaji mwingi jambo linalozua migogoro mingi na kumwomba Waziri wa Ardhi,Deogratius Ndejembi kumtumia orodha ya migogoro sugu ili baada ya kampeni hiyo waanze kuishughulikia.
"Kupitia kampeni hiyo tulifika katika mikoa 11 na changamoto zilizojitokeza kwa wingi ni ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi, ndoa na ardhi,katika sera yetu ya utoaji haki tutahakikisha wananchi wanapata haki na wanapata elimu ya kisheria,"amesema.
Amesema watu wa pembezoni wana kiu ya haki ndio maana Rais aliunda Tume ya Haki jinai ambayo ilibainisha umuhimu wa haki kumfikia kila Mwananchi.
"Kupitia kampeni hiyo tuliweza kuwafikia watu 175,119 ambapo asilimia 49 ni wanawake na 51 ni wanaume ambapo tulitatua jumla ya migogoro 3162,takwimu hizi zinaonesha wanaume ni wengi kuliko wanawake ni takwimu nzuri tu,unaona Mpango huu unamsaidia Mwananchi kuzalisha zaidi, programu hii ni mkombozi kwa wanyonge hasa wale ambao hawana uwezo wa kupata mawakili,"amesema Waziri Ndumbaro
Waziri huyo pia amesema mpango huo utamsaidia mnyonge kupunguza malalamiko katika sekta ya sheria na kwamba Januari 24 mwaka huu watazindua kampeni hiyo kwa mikoa 6 Mkoani Kigoma.
"Mikoa mingine itakayofikiwa ni,Kilimanjaro,Geita,Katavi,Tabora na Mtwara,katika mikoa hiyo tutakuwa Januari tu na katika Kila Halmashauri wataenda Kata 10 katika Kila Kata watatumia siku 9 na huduma zitatolewa bure kwa wananchi,"amesema
Social Plugin