Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NI WAZI! DR. SAMIA, DR. HUSSEIN MWINYI KUGOMBEA URAIS 2025




Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) leo tarehe 19 Januari 2025 wamepitisha kwa kauli moja Azimio la kuwaridhia Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, kugombea tena nafasi zao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ametoa ushauri muhimu kuhusu umoja na uwazi ndani ya chama.

Kikwete amesisitiza umuhimu wa kufuata utaratibu rasmi wa chama kwa kupitisha azimio la kuidhinisha majina ya viongozi hao kama wagombea wa urais.

 Ameweka wazi kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao hauwezi kutiliwa shaka kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia na Rais Mwinyi.


“Kama tumekubaliana katika mkutano huu, basi Rais Samia na Rais Mwinyi wanaelekea kuendelea kushika madaraka kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Hata hivyo, ni muhimu tupitishe azimio hili ili tuzingatie kanuni za chama na kuonyesha mshikamano kwa wanachama wetu wote,” amesema Kikwete.


Azimio hilo limezingatia Ibara ya 100(2) ya Katiba ya CCM, inayotaja kwamba Mkutano Mkuu wa CCM ndio chombo cha juu chenye mamlaka ya mwisho katika maamuzi makubwa ya chama.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu walijadili utekelezaji wa Ilani ya CCM, wakionesha kuridhishwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi. Kufuatia hoja zilizowasilishwa, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilichukua jukumu la kuandaa Azimio hilo na kulipeleka kwa Mkutano Mkuu ulioketi katika Ukumbi wa JKCC, Dodoma, ambapo wajumbe wote waliridhia kwa asilimia 100.

Kwa kauli moja, wajumbe wameonesha mshikamano na imani kubwa kwa viongozi hawa, wakisifu juhudi zao za kuboresha maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com