Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO NA NGUVU YA VYAMA VYA USHIRIKA NCHINI – DKT. NINDI




Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi,akizungumza leo Januari 10,2025 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ( 1992) LTD cha kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maendeleo ya ushirika nchini.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI inatambua mchango na nguvu ya Vyama vya Ushirika katika kuchochea na kuwawezesha kiuchumi watu wenye kipato kidogo katika jamii, wazalishaji, wakulima wadogo, wanawake na vijana, ambao vinginevyo wasingeweza kuhimili ushindani kwenye soko kama wanavyoweza wafanyabiashara binafsi.

Hayo yamesemwa leo Januari 10, 2025 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi, wakati akifungua Kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ( 1992) LTD kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maendeleo ya ushirika nchini.

Dkt.Nindi, amewataka kuendeleaa kuwawezesha wananchi wenye mitaji midogo kuwekeza pamoja katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kumiliki nyenzo za uzalishaji na biashara.

"Endeleeni kuwezesha Wananchi kuingia na kushiriki katika shughuli kuu za uchumi wa nchi kama vile Viwanda na mabenki pamoja na kuwaunganisha Wananchi na kujenga uhusiano na misingi ya Utawala bora na demokrasia," amesema Dkt.Nindi.

Aidha, amevitaka Vyama vya Ushirika kuwapatia wananchi wengi wa kawaida fursa ya kunufaika na mitaji midogo ya kuendeshea biashara kupitia Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), ili waweze kupunguza umaskini.

Amesema Serikali inaendelea kuunga mkono mikakati ya wanaushirika na Tume ya Maendeleo ya Ushirika pia, vikiwemo vipaumbele vilivyoelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume kuhakikisha vinaleta matokeo yanayotarajiwa.

Pia Dkt.Nindi ameipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika kwa kuandaa kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ambacho ni muhimu.

Amesema kuwa ni matarajio yake kwamba kikao hicho kitatoa Dira na uelekeo wa Ushirika nchini kupitia Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini.

“Nizipongeze Bodi za TFC na SCCULT kwa kuteuliwa kwao ili kusimamia uendeshaji wa Taasisi hizi. Ni matarajio ya Wizara kuwa, Uongozi huu utaleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Ushirika nchini.

“Kwa taarifa ya Mrajis, inaonesha kwamba uteuzi wenu, umezingatia weledi na uzoefu, hivyo ni rai yangu kwenu mtumie uwezo wenu wote kuhakikisha Taasisi hizi zinakuwa chachu ya Maendeleo ya Ushirika nchini,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema lengo la kikao kazi hicho ni kukutanisha Bodi za Taasis hizi mbili, ili kujadili kuhusu mienendo ya Taasis hizo, baada ya kaguzi na ufuatiliaji mbalimbali kwa muda sasa kubainisha udhaifu wa uendeshaji wake.

“Kimsingi Taasis hizi zilianzishwa kwa madhumuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushawishi na utetezi wa vyama na wanachama wao, uwakilishi wa vyama wanachama kwenye majukwaa ya ndani na nje ya nchi, kuunganisha vyama vya ushirika na masoko, kuwajengea uwezo vyama wanachama, pamoja na kuwaunganisha wanachama na Taasisi za Fedha,” amesema Dkt. Ndiege

Aidha, amesema pamoja na majukumu hayo muhimu waliokuwa nayo, utendaji wa taasisi hizi kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano mfululizo umekuwa ni wa kusuasua, jambo linalopelekea wanachama na wadau wengine kukosa imani na uendelevu wa Taasis hizo.

“Kwa kushirikiana na wenzangu, tulitafakari kuhusu uendeshaji wa Taasis kama hizi katika nchi zinazofanya vizuri kwa upande wa Ushirika, kama vile Japan, Malaysia, Indonesia, Nigeria, India, ili kujifunza na kupata uzoefu kuwa wenzetu wanafanyaje.

“Nimejifunza kuwa baadhi ya nchi duniani, mashirikisho na miavuli yamekuwa ni chachu ya ukuaji wa ushirika katika nchi zao, na watetezi wakuu wa vyama wanachama katika masuala mbalimbali, kwa kutekeleza majukumu mbalimbali,” amesema.

Dkt.Ndiege amesema katika nchi nyingine pamoja na masuala mengine, serikali inagharamia uendeshaji wa Taasisi hizo ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya watumishi.

“Hivyo, kwa uzoefu huo ni matarajio yetu kuwa serikali yetu ina matarjio makubwa sana kwa Taasis hizi kama miavuli ya Vyama vya Ushirika nchini, katika kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine, vyama na Wadau mbalimbali vinatafutiwa fursa za kiuchumi za ndani na nje ya nchi, badala ya serikali kufanya shughuli hizo moja kwa moja,” amesema.

Kadhalika, amesema kwa sasa kuna jumla ya vyama vya ushirika 6,570 wananavyosimamia ambavyo kati ya hivyo, TFC na SCCULT ni miongoni mwao, ambavyo vinayo majukumu ya kuwakilisha Vyama wanachama wao kitaifa na kimataifa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya TCDC Bi. Irene Madeje, ameipongeza uamuzi wa kuitisha kikao hicho muhimu, ambacho kama alivyoelezea Mrajis, kimelenga kushirikishana mienendo ya Taasis hizi ili kupokea maelezo ya Serikali kwa Bodi Mpya baada ya kuteuliwa, ili kuleta mabadiliko yatakayosaidia kuleta matokeo chanya kwa Maendeleo ya Ushirika nchini.

"Niwapongeze wateule wote kwa imani ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika kwenu. Sisi tunatarajia makubwa kutoka kwenu ikizingatiwa kuwa wateuliwa wametokana na kada mablimbali, zikiwemo; uchumi, sheria, uongozi." amesema Bi.Madeje.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi,akizungumza leo Januari 10,2025 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ( 1992) LTD cha kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maendeleo ya ushirika nchini.


Mrajis na Mtendaji Mkuu Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege,akizungumza wakati wa Kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ( 1992) LTD cha kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maendeleo ya ushirika nchini.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Kikao kazi cha TCDC, TFC na SCCULT ( 1992) LTD cha kutoa mwelekeo wa serikali kuhusu maendeleo ya ushirika nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com