Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TASAC YAAGIZWA KULINDA USALAMA WA WANANCHI MAJINI

Na Mwandishi Wetu, MWANZA.

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameliagiza Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuendelea kununua boti na vifaa vya kisasa vya uokoaji ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi majini kwa usalama zaidi.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati alipokagua ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria kinachojengwa na TASAC.

Alisema pindi ajali za majini zinapotokea, shughuli za uokoaji zinachelewa kufanyika kwa wakati kwa sababu ya kukosekana vifaa vya kisasa vya uokozi.

"Tunahitaji Watanzania katika maeneo ya maziwa na hata Bahari ya Hindi wafanye shughuli zao kwa usalama zaidi, hivyo vifaa vya kisasa vya uokoaji ni muhimu," Profesa Mbarawa alisema.

Kadhalika, aliipongeza TASAC kwa kusimika minara na vifaa vya mawasiliano katika Ziwa Victoria ambavyo vitasaidia pindi ajali za majini zitakapotokea.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Hamid Mbegu, alisema tayari shirika hilo limeanza kutekeleza agizo hilo kwa vitendo ambapo katika mwaka huu wa fedha TASAC imepanga kununua boti mbili za uokoaji.

"Na katika mwaka ujao wa fedha tumepanga kununua boti tatu za uokoaji ambapo jumla tutakuwa na boti tano. Tumezingatia viwango vya kisasa," Mbegu alieleza.

Mratibu wa mradi huo, Nahodha Emmanuel Marijani, alisema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 70 ambapo kinajengwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.

Pia, alisema vituo vingine vitatu vya utafutaji na uokoaji vimejengwa katika Bandari ya Musoma, Nansio na Kanyala.

Alibainisha kuwa mbali na ujenzi wa vituo hivyo, boti tatu ambazo ni za utafutaji na uokoaji pamoja na kubeba majeruhi, zitanunuliwa.

"Leo usiku wataalamu wetu wataanza safari kwenda Uturuki kwa ajili ya kuifanyia majaribio ya mwisho 'Ambulance boat' na baada ya hatua hiyo italetwa nchini," alieleza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com