Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Khamis amesema Tume inaendelea kutuma njia mbalimbali za kutoa elimu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili wananchi waweze kutambua haki na wajibu wao.
Hayo ameyasema Januari 23, 2025 wakati akitoa elimu hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kinampanda, Wilaya ya Ilamba Mkoani Singida.
Akitoa elimu kuhusu haki za binadamu na utawala bora, Mhe. Mohamed amesema kuwa Serikali ina dhamira nzuri ya kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kuanzisha Ofisi ya THBUB yenye dhamana ya kuendeleza dhamira hiyo kwa kutekeleza majukumu yake ambayo yameainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
"Ibara ya 12 mpaka ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeainisha haki mbalimbali ambazo ukizivunja Sheria inachukua mkondo wake" amesema Mhe. Mohamed
Aidha, Mhe. Mohamed ametoa wito kwa jamii kutimiza wajibu wao ili wasikinzane na Sheria.
“Haki inaenda na Wajibu, ni wajibu wa kila mmoja kutii Sheria zilizowekwa” amesisitiza Mhe. Mohamed.
Kwa upande wao, wakazi wa Kata ya Kinampanda waiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuendelea kutoa elimu juu ya Haki za Binadamu na misingi ya Utawala Bora.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Samson Mpanda amesema kuwa wananchi wengi hawajui haki zao kama vile haki ya kujieleza na kutoa maoni, haki ya kumiliki mali na haki nyingine.
"Utakuta mtu anakamatwa anapokwonywa mali kutokana na kutojua haki zake" amesema Bw. Mpanda
Social Plugin