Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UUNGANISHAJI UMEME VIJIJINI WAFIKIA ASILIMIA 99.9



Na mwandishi wetu, Dar

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umesema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba 2024, vijiji vilivyounganishwa na umeme nchini vimefikia 12,301 kati ya vijiji 12,318 ambayo ni sawa na asilimia 99.9.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 5 Januari, 2025 na Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mha. Jones Olotu wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya upatikanaji umeme vijijini kwa Wanahabari tulipotoka, tulipo na tunapokwenda kuelekea Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati jijini Dar es Salaam.

"Vijiji 17 vilivyobakia wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa miundombinu na vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi januari mwaka 2025," amesema Mha. Olotu.

Ameongeza kuwa, Tanzania Bara ina jumla ya vitongoji 64,359 ambapo tayari vitongoji 33,657 sawa na asilimia 52.3 vimefikiwa na umeme na vitongoji 30,702 vilivobaki vipo kwenye mpango wa kupatiwa umeme kwa kipindi cha miaka mitano.

Vile vile, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imefanikiwa kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi maeneno ya vijijini kwa kuwatengenezea fursa za uwekezaji kwa kutumia huduma ya umeme.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaotarajiwa kufanyika januari 27 - 28 na kuhudhuriwa na watu wasiopungua 1,500 kutoka nchi mbalimbali.

Miongoni mwa washiriki ni Wakuu wa Nchi za Afrika, Mawaziri wa Nishati na Fedha, Mabalozi, Taasisi za Kimataifa, Makampuni yaliyowekeza kwenye sekta ya Nishati na watafiti.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com