Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANA-GDSS WAJADILI NA KUWEKA MIKAKATI YA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MAONI RASIMU YA DIRA YA TAIFA 2025-2050


Washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) leo Jumatano, Januari 22, 2025, wamejadili masuala mbalimbali yanayohusiana na rasimu ya Dira mpya ya Taifa 2025-2050 katika semina iliyofanyika katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Mwanasaikolojia Sylvia Sostenes ameibua hoja kuhusu umuhimu wa masomo ya stadi za kazi katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia kipato na kuwasaidia kufanikisha mahitaji ya familia, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto shule.

Hata hivyo, ameeleza kuwa mfumo wa elimu wa sasa unakazia zaidi nadharia badala ya ujuzi wa vitendo, hali inayowafanya wahitimu wengi kukosa uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuhalisia kazini.

Sylvia amesisitiza kuwa kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya miaka 25 ijayo, ili kuhakikisha kuwa wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya kati wanakuwa wajasiriamali, watengenezaji wa ajira, au wataalamu wa vitendo badala ya kutegemea tu kuajiriwa.

Kwa upande wake, Shiganga George ametoa wito kwa wananchi kufuatilia sera za vyama vya siasa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu, kuhakikisha sera hizo zinaendana na maono ya Dira ya Taifa 2020-2025.

Shiganga ameendelea kwa kusema kuwa, hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wa kisiasa na kufanikisha utekelezaji wa dira ya maendeleo.

Naye Msafiri Mwajuma ameeleza kuwa Dira ya Taifa inapaswa kutambulika kama tunu ya taifa na kuingizwa kwenye ilani za vyama vya siasa, ili utekelezaji wa sera za serikali uwe na mwelekeo mmoja wa maendeleo.

Msafiri ameonya dhidi ya viongozi wanaoibua dira mpya kila baada ya uchaguzi.

Mariam Machicha yeye kwa upande wake, amewataka wananchi kufuatilia bajeti za serikali kwa makini, akisema kuwa bajeti hizo hutoa taarifa muhimu kuhusu utekelezaji wa mipango na mwelekeo wa maendeleo ya taifa kwa mwaka ujao.

Aidha, imebainika kuwa sekta ya afya, kama ilivyoainishwa kwenye rasimu ya Dira ya Taifa 2025-2050, inaonesha maendeleo mazuri.

Hata hivyo, hoja zilitolewa kuhusu ukosefu wa mikakati mahsusi kwa watu wasioweza kugharamia huduma za afya.

Pia, sekta binafsi imeonekana kuwekewa mazingira mazuri kwa mujibu wa dira hiyo.

Semina ya leo imeendeshwa chini ya mada kuu ya "Mapitio ya Rasimu ya Dira Mpya ya Taifa na Mikakati ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Maoni Yaliyotolewa" ikihitimishwa kwa kusisitiza mshikamano wa kitaifa na uwajibikaji wa pamoja kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com