Wananchi wa kijiji cha Liweta katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, wameishukuru Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kukamilisha ujenzi wa daraja la kudumu katika mto Liweta.
Daraja hili linaunganisha kijiji hicho cha Masuku, hivyo kuwaondolea changamoto kubwa ya mawasiliano, hasa wakati wa masika.
Wamezungumza kwa nyakati tofauti, wananchi Wamesema kuwa hapo awali walikabiliwa na changamoto ya kusubiri siku kadhaa maji yapungue ili kuvuka mto na kufika vijiji jirani au mashambani.
Michael William amebainisha kuwa hali hiyo ilisababisha ucheleweshaji wa shughuli za kilimo na kupunguza kipato chao wananchi Wamesema kuwa maisha yao sasa yameimarika kutokana na uwepo wa daraja hilo.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea, Mhandisi Godfrey Mngale, amesema Serikali imetumia Shilingi milioni 449 kukamilisha mradi wa daraja hilo pamoja na upanuzi wa barabara.
Amesema kuwa daraja hilo si tu limeimarisha mawasiliano, bali pia litarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka mashambani kwenda sokoni.
Wananchi wamesisitiza umuhimu wa barabara hiyo kuboreshwa zaidi ili kufika maeneo yenye uzalishaji mkubwa kama Litapatile.
Malaika Komba ni mkazi wa kijiji cha Masuku, amesema awali walikuwa wakikabiliwa na mateso makubwa, ikiwa ni pamoja na kupoteza mazao na hata ndugu kutokana na mafuriko wakati wakivuka mto.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo, amesema daraja hilo lina urefu wa mita 20 na njia nne za kupitisha maji.
Ameongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia mpango wa kuondoa vikwazo vya usafirishaji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kwa ujumla, wananchi wa Liweta na Masuku wamefurahia ujenzi wa daraja hilo na wameahidi kulinda miundombinu hiyo muhimu kwa kutojihusisha na vitendo vya uharibifu kama vile kuchimba mchanga na kuiba alama za barabarani. Serikali ya awamu ya sita imetajwa kuwa mkombozi mkubwa wa changamoto za miundombinu katika maeneo ya vijijini.
Social Plugin