Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUFANYA UTAFITI WA HALI YA UPATIKANAJI NA MATUMIZI YA NISHATI

Wananchi wa Kitongoji cha Mpazu Wilaya ya Iramba Mkoani Singida wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kufanya utafiti wa hali ya upatikanaji na matumizi ya nishati. ya wilayani humo.

Wametoa pongezi hizo Januari 19, 2025 kwa nyakati tofauti baada ya kufanyiwa mahojiano ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika utekelezaji wa tafiti hiyo.

Walisema kuwa hatua hiyo ya utafiti inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuweka mipango thabiti ya kuwasogezea huduma muhimu za nishati wananchi wake.

"Tunaipongeza Serikali kwa kufanya utafiti huu, tunaamini matokeo ya utafiti huu yatazalisha miradi itakayotuondolea adha mbalimbali tulizonazo," alisema Gabriel Ndabo.

Alisema kumekuwepo na changamoto ya ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuni na kwamba kupitia utafiti huo, Serikali itaweka mkakati imara wa kulinda misitu.

Naye Juliana Mtuwa alisema kwa sasa wanatumia zaidi kuni kupikia na kwamba madhara yatokanayo na matumizi ya kuni ni mengi ikiwemo kusababisha madhara ya kiafya.

"Tunachangamoto, tunahitaji maendeleo na utafiti huu ni hatua muhimu ya maendeleo," alisema Bi Mtuwa.

Aliongeza kuwa tarafa hiyo haijafikishiwa umeme na kwamba wanafunzi wanapata tabu kujisomea hivyo kupitia tafiti hiyo Serikali itapata mwanga wa hali halisi ilivyo.

Akizungumzia utekelezaji wa utafiti huo, Mdadisi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bi Gloria Nkungu alisema huo ni utafiti wa tatu anashiriki na kwamba akilinganisha utafiti uliyopita na huu kuna hatua imepigwa.

"Huu ni utafiti wa tatu wa Nishati ninashiriki, tunaendelea vizuri wananchi wanatupa ushirikiano na kwa baadhi ya maeneo tumeshuhudia mabadiliko makubwa," alisema Bi Nkungu.

Serikali inafanya utafiti wa upatikanaji na matumizi ya nishati katika mikoa yote Tanzania Bara kwa lengo la kubaini hali ya usambazaji na matumizi ya nishati ili kuboresha maisha ya wananchi wake kupitia sekta ya nishati.

Zoezi hili la ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya tafiti ya upatikanaji na matumizi ya nishati lilianza tangu mwezi Desemba 2024 na linatarajia kuhitimishwa mwezi Januari 2025 ili kuendelea na uchakataji wa takwimu zilizokusanywa na Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kutoka mwezi Machi 2025.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com