Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
Wadau wa sekta ya uvuvi nchini wamekutana leo jijini Dodoma kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta hii muhimu.
Kikao hiki cha wadau kilihusisha viongozi kutoka serikalini, wataalamu wa uvuvi, na wawakilishi kutoka kwenye taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.
Mkurugenzi wa uvuvi katika Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Betrece Marwa, ameeleza kuwa hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi na kwamba ni itasaidia kukuza, kuendeleza na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba .
Amesema ufugaji samaki kwa kutumia njia hiyo ya vizimba ni mojawapo ya mbinu muhimu ya kupunguza uvuvi haramu na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji ikiwa ni pamoja na uhifadhi ardhi na mazingira kwa ujumla.
Mbali na hayo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia juhudi zinazofanywa na serikali katika kuweka mazingira bora ya kazi na uwezeshaji wa wafugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji na ubora wa samaki wanaozalishwa.
Katika kikao hicho, wadau walijadili pia mbinu mbalimbali za kuboresha ufugaji wa samaki na namna ya kuongeza uzalishaji wa samaki, hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa rasilimali za maji.
Vilevile, wadau hao wamesisitiza umuhimu wa kushirikiana ili kuhakikisha rasilimali za majini zinatumika kwa manufaa ya taifa na kwamba uchumi wa sekta ya uvuvi uendelee kukua, huku ukizingatia utunzaji wa mazingira na ustawi wa jamii zinazotegemea shughuli hizo.
Pia, wamejadili mikakati ya kuhakikisha wananchi wananufaika na ufugaji wa samaki kwa vizimba, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu za mafunzo kwa wakulima na wavuvi ili kuboresha ufanisi wa shughuli zao.
Lengo ni kuwa na mfumo endelevu utakaosaidia kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa maeneo mbalimbali nchini.
Social Plugin