Wananchi na jeshi la polisi Kahama wakishuhudia mwili wa mwanamke uliofukuliwa baada ya kuuawa na kuzikwa katika shimo
NA NEEMA NKUMBI- KAHAMA
Mwili wa Mwanamke Asha Mayenga anayekadiriwa kuwa na miaka 62 uliozikwa Malindi Mtaa wa Seke Kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama baada ya kuuawa umefukuliwa na Jeshi la polisi huku ndugu wa marehemu wakiutambua mwili huo.
Tukio la kufukua kaburi limefanyika Januari 17, 2025 ambapo Mwenyekiti wa mtaa wa Seke Christopher Robart ameeleza kuwa alipewa taarifa na balozi kuhusu tukio hilo Januari 16, 2025 saa 10 jioni na kutoa taarifa polisi.
"Jana majira ya saa kumi nilipigiwa simu na balozi kwamba kuna tukio huku, nilipofika katika eneo hilo tulipewa taarifa na polisi kwamba tulinde eneo hilo ndipo polisi wamekuja leo na kufukua shimo hilo na kukuta mwili wa mwanamke", amesema Christopher.
Mume wa marehemu Mashauri Mlekwa amesema alipewa taarifa za mke wake kupotea siku ya Jumatatu alipoenda shambani kulima na vijana wake ambapo vijana hao walirudi lakini bibi huyo hakuonekana.
Mashauri amesema vijana hao waliporudi walihamisha vitu vya marehemu na kuuza baadhi ya magunia ya mpunga huku mmoja wa vijana hao kuondoka kwenda Katoro.
"Nilipewa taarifa na mtoto wangu za kupotea kwa mke wangu siku ya Jumatatu alipokuwa ameenda kulima na vijana wake, vijana hao walirudi ila mke wangu hakurudi, nilichukua jukumu la kumtafuta bila mafanikio ndipo nikaenda polisi kutoa taarifa polisi," amesema mzee Mashauri.
Shuhuda wa tukio hilo Juma Dutu ameeleza kuwa alipewa taarifa na wachungaji wake wa ng'ombe wakiwa wanachunga, ng'ombe wale walienda na kuzingira eneo hilo ndipo wachungaji hao walipoenda kuwafukuza na kugundua kuwa kuna kitu kimefukiwa.
"Wachungaji wangu wa ng'ombe walikuwa wanachunga katika maeneo haya ndipo ng'ombe walikimbilia eneo hilo na kuanza kufukua, wachungaji wangu waliwapiga ng'ombe ili watoke ndipo walipogundua kwamba kuna kitu kimefukiwa na kuja kunipa taarifa", amesema Juma.
Naye kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza chanzo cha kifo cha mwanamke huyo ni mgogoro wa ardhi baina yake na mtoto wake.
Kamanda Magomi ameongeza kuwa tukio hili ni la kikatili hivyo wanawashikilia watu watatu kwa ajili ya upelelezi akisema kuondoa uhai wa mtu mwingine ni kosa la jinai.
"Tukio hili la kuondoa uhai wa mtu ni la kikatili sana, sisi jeshi la Polisi tutasimamia vizuri upelelezi na tutahakikisha kwamba waliohusika tunawapeleka katika vyombo vya sheria", amesema RPC Magomi.
Wananchi na jeshi la polisi Kahama wakishuhudia mwili wa mwanamke uliofukuliwa baada ya kuuawa na kuzikwa katika shimo
Wananchi na jeshi la polisi Kahama wakishuhudia mwili wa mwanamke uliofukuliwa baada ya kuuawa na kuzikwa katika shimo
Social Plugin